Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatarajiwa kuanza utekelezaji Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma kwa kuanza kuhamasisha wananchi wa kata za Mpunguzi na Matumbulu kufanya maendeleo kwa kuzingatia mpango huo.
Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Bi. Imaculate Senje ilikutana na Wenyeviti wa Mitaa iliyo kwenye kata hizo kwa lengo la kuwajengea ufahamu kuhusiana na utekelezaji Mpango Kabambe.
Akizungumza na Wenyeviti hao leo tarehe 20 Januari 2021 katika ofisi ya Mtendaji Kata ya Matumbulu jijini Dodoma, Bi Imaculate alisema Wizara kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Dodoma imeamua kuanza uhamasishaji wa utekelezaji wa mpango huo ili wananchi waulewe na kuachana na ile dhana ya kusema Serikali inapora maeneo.
Mkurugenzi huyo Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, zoezi la utekelezaji Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma unalenga maendelezo ya eneo hilo kufanyika kwa kuzingatia mpango huo.
Kwa mujibu wa Bi. Imaculate, kwa kuanzia utekelezaji Mpango Kabambe utaanzia kata ya Mpunguni na kuhusisha maeneo ya Mashamba na Viwanda na baadaye katika maeneo ya makazi ya wananchi ambapo zoezi litakalofanyika huko ni la urasimishaji.
‘’Kipaumbele kwa sasa katika zoezi la utekelezaji mpango kabambe wa jiji la Dodoma litakuwa katika maeneo ya mashamba na viwanda na hapa tunataka tuepuke ujenzi holela katika maeneo hayo na kuzingatia mpango kabambe uliopo’’ alisema Imaculate.
Alisema, wakati wa utekelezaji zoezi hilo hatua ya awali wataalamu watachukua taarifa za wamiliki wote kwenye maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya mashamba na viwanda ambapo maeneo hayo yatapimwa na wamiliki wake kumilikishwa na kusisitiza kuwa, baada ya kumilikishwa hawataruhusiuwa kufanya maendelezo kinyume na mpango kabambe.
Kwa upande wake Afisa Mipango Miji wa halmashauri ya Jiji la Dodoma Aisha Masanja alisema lengo la kukutana na wenyeviti wa mitaa kabla ya kukutana na wananchi ni kuwataka wenyeviti hao kuwa mabalozi wazuri wa kuwaelimisha wananchi kuhusiana na zoezi hilo na kuongeza kuwa inachotaka serikali kupitia zoezi hilo ni kuhakikisha kila mwananchi anabaki katika eneo lake na kusisitiza kuwa baada ya hapo itatolewa ramani ya msingi itakayoainisha shughuli ya kila eneo kulingana na mpango.
Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma ulizinduliwa Februari mwaka 2020 na Waziri Mkuu Mhe. Kasim kwa ajili ya kulifanya jiji la Dodoma kuwa bora na la Kisasa.