NEWS

25 Machi 2021

Makamu Wa Pili Wa Rais Zanzibar Aongoza Wakazi Wa Geita Na Mikoa Jirani Kumuaga Hayati Dkt. John Pombe Magufuli


Na Mwandishi Wetu, Geita
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amewaongoza wakazi wa Geita na mikoa jirani kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli katika uwanja wa Magufuli Chato mkoani Geita.

Akizungumza katika shughuli hiyo ya kuuaga mwili wa hayati Magufuli Wilayani Chato, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa kamati ya mazishi kitaifa amewasihi Watanzania kuendelea kushikamana katika kulijenga taifa, ambalo Magufuli ameliacha salama na lenye heshima.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, amesema ni wajibu wa viongozi na Watanzania kuungana kuenzi mazuri yote aliyofanya Hayati Magufuli na kuendeleza sera zake za kuchapa kazi, kupiga vita rushwa na ubadhirifu na kuweka mbele uzalendo na maslahi ya taifa.

Mazishi ya Hayati Dkt. Magufuli yatafanyika Ijumaa Machi 26, 2021 katika makaburi ya familia kijijini kwake Chato mkoani Geita.