NEWS

25 Machi 2021

Wanafamilia Watano Wanaodaiwa Kufariki Wakati Wa Kuaga Mwili Wa Hayati Dr Magufuli Kuzikwa Leo Dar es Salaam

 Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu na mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori wameongoza mamia ya waombolezaji katika ibada ya mazishi ya familia ya ndugu watano wanaodaiwa kufariki kwa kukanyagwa katika shughuli ya kuaga mwili wa marehemu  John Magufuli katika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.


Ndugu hao wa familia ya Daudi Mtuwa ni  Susan Mtuwa na watoto wake wawili Nathan (6) na Natalia (5) pamoja na watoto wengine wawili Cris (11) na Michelle (8) wa shemeji zake Susan walifariki dunia katika shughuli hiyo iliyofanyika Jumapili Machi 21, 2021.

Akizungumza katika maombolezo hayo, Mtemvu amesema kuwa kazi ya Mungu haina makosa na kila kifo kina sababu zake.

Watoto hao wanatarajia kuzikwa leo saa 10 jioni eneo la nyumbani kwa Mtuwa, Kimara mkoani Dar es Salaam.