NEWS

30 Aprili 2021

Dkt. Zainab Chaula Afungua Mafunzo Ya Matumizi Ya Mobile App Ya Mfumo Wa Anwani Za Makazi Na Postikodi

Na Prisca Ulomi, WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula amefungua mafunzo ya programu tumizi (mobile app) ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi kwa watendaji 175 wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, halmashauri za  Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela na wenyeviti wa Serikali za Mtaa wa Halmashauri hizo mkoani Mwanza

Dkt. Chaula amefungua mafunzo hayo ya kujenga uelewa kwa watendaji hao ili kufanikisha utekelezaji, matumizi na manufaa ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi ambapo mfumo huu utawawezesha watendaji wa Serikali ya Mtaa kuwa na taarifa za wakazi kiganjani kwa kuwa kila mwananchi atafahamika nyumba na mtaa anaoishi na kila mwananchi atakuwa na anwani ya makazi ya mahali alipo iwe mahali pa kazi, ofisini au biashara hivyo kuwezesha upatikanaji, upokeaji na upelekaji wa huduma kwa wananchi

“Mtu akiamka kitandani kitu cha kwanza anaangalia simu kuona je ametafutwa, kuna ujumbe wowote hivyo hii inaonesha mawasiliano ni jambo la msingi katika kipindi hiki tofauti na miaka ya nyuma ambapo mawasiliano yalionekana ni anasa na sasa programu tumizi (mobile app) ya mfumo huu itarahisha utambulisho wa watu, kuwezesha utambuzi wa mwelekeo na maeneo ambapo mtu anataka kwenda,   kuwezesha biashara mtandao, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kufanikisha usalama wa nchi”, amefafanua Dkt. Chaula

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kuwa postikodi ni jambo muhimu kwa maendeleo ya taifa na ana imani na Dkt. Chaula kuwa kazi hii sasa ya kuweka miundombinu ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi unafika mwisho.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa utekelezaji wa mfumo huu unaendelea kwenye Halmashauri ya jiji la Mwanza na ya Manispaa ya Ilemela ambapo Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam inaweka nguzo za majina ya mitaa zipatazo 5,300 na vibao vya namba za nyumba 92,796 kwenye kata 18 na kazi imeanza kutekelezwa mwezi Februari, 2021 na itakamilika kwa muda wa kipindi cha miezi sita kwa gharama ya shilingi 1,357,356,832

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichalwe aliwaeleza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuwa TEHAMA ni mwambata wa Sekta ya Afya na mifumo yake inatumika kuhudumia wananchi kwa kuwapatia matibabu, vipimo, dawa, vifaa tiba na vitendanishi, bima ya afya hivyo TEHAMA inaboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hivyo amewataka wasimamie utekelezaji wa mfumo huu kama wanavyofanya kwenye sekta nyingine za elimu na maji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Afisa Mipango wa Jiji hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya utekelezaji ya mfumo huu, Moses Seleki amemhakikishia Dkt. Chaula kuwa Mwanza watashirikiana vema na viongozi wao wa Serikali za Mitaa kutumia na kulinda miundombinu hii
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nela, Abubakari Seif akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake wa Serikali za Mitaa, amesema kuwa Serikali imewathamini kwa kuwapatia mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu mfumo huu kwa kuwa anwani za makazi na postikodi ni suala la ulinzi na usalama, uchumi, kodi ya ardhi, bima ya afya na majanga ya moto hivyo Tanzania imeingia kwenye hatua kubwa ya maendeleo kwa kutumia anwani za makazi na postikodi

Pia, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi pamoja  na wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Seveline Lalika wamemweleza Dkt. Chaula kuwa watatoa kipaumbele kwa kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mfumo huu kwenye maeneo yao ili Jiji la Mwanza liwe la mfano wa kuigwa nchini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari