NEWS

27 Aprili 2021

Serikali Kuandaa Mkakati Wa Udhibiti Wa Athari Za Zebaki


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amesema Serikali kwa kushirikiana na mamlaka husika itaandaa Mkakati wa udhibiti wa athari za zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira.

Jafo amesema hayo leo Aprili 27 wakati akiwasilisha Hotuba ya Mapato na   Matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni jijini Dodoma.

Alisema sambamba na hayo itaainisha na kufanya tathmini ya maeneo yenye shughuli nyingi za uchimbaji mdogo wa dhahabu kwa kutumia zebaki na kuweka mikakati ya kuyarejesha katika hali yake ya asili.

Aidha, waziri huyo aliongeza kuwa katika kutekeleza Mpango-kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini Serikali itatoa mafunzo kwa mamlaka zinazohusika na udhibiti wa zebaki kuhusu namna ya kudhibiti uingizaji, matumizi na utupaji wa taka zitokanazo na zebaki nchini.

Katika hotuba hiyo pia alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa kuandaa Mkakati wa Nishati Mbadala ya Kuni na Mkaa kwa ajili ya kupikia na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya nishati mbadala.

“Mheshimiwa Spika tutaendelea kutoa elimu ya nishati mbadala hususan hususan kwa taasisi zinazotumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia zikiwemo magereza, polisi, na taasisi za elimu. Katika kipindi hiki, Ofisi itaendelea na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango iliyowekwa na taasisi mbalimbali kuhusu matumizi ya nishati mbadala,” alisema.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Eric Shigongo alishauri Ofisi ya Makamu wa Rais ishirikiane na Ofisi ya Mkemia Mkuu kudhibiti uingizwaji wa zebaki nchini.

Katika hotuba hiyo aliyoiwasilisha kwa niaba ya Mwenyekiti Mhe. David Kihenzile alishauri Serikali itafute teknolojia mbadala ambayo wachimbaji hao wataitumia ili kuachana na matumizi ya zebaki.

“Uingizaji holela na utumiaji wa kemikali ya Zebaki nchini kutokana na kuwapo kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu wanotumia kemikali hiyo, unaathiri kwa kiasi kikubwa afya na usatwi wa wchimbaji hao. Madhara ya matumizi ya kemikali hiyo yanatokana na wachimbaji wengi kuitumia bila ya kuwa nyenzo za kujinga kutokana na zebaki,” alisema.

Shigongo ambaye pia ni Mbunge wa Buchosa alitahadharisha kuwa maji yanayotumika kusafishia dhahabu yakiwa yamechanganyika na Zebaki, yanatiririkia kwenye vyanzo vya maji na kuwa watu wanapotumia maji hayo.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Hawa Mchafu alishauri Serikali itumie fedha kutoka mifuko ya mazingira kwa kusaidia katika kujenga uelewa wa kupunguza matumizi ya zebaki.

Pia Mbunge huyo alipendekeza njia mbadala ya matumizi ya zebaki na kusema kuwa kemikali hiyo ina athari kubwa kwa binadamu hususan katika maeneo ya Kanda ya Ziwa ambako kuna shughuli za uchimbaji wa dhahabu.