Wanafunzi wa sayansi ya madini ya vito kutoka kituo cha Jemolojia Tanzania kilichopo mkoani Arusha wamesema elimu ya uongezaji thamani madini wanayoipata kupitia kituo hicho inawapa uhakika wa maisha yao ya badaye kutokana na kuwa na wigo mpana wa kujiajiri na hata kuajiriwa.
Akizungumza wakati wa mahojiano na maafisa habari kutoka Idara ya Habari Maelezo waliofika kituoni hapo ili kujionea mwenendo mzima wa mafunzo hayo, mwanafunzi Lightness Makundi alisema elimu anayoipata inamsaidia katika kutambua na kuthaminisha aina za madini ya vito, itamsaidia kutambua madini halisi na madini fake na hivyo kutopata hasara endapo ataamua kujiingiza katika kufanya biashara ya madini mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo.
Amesema elimu ya sayansi ya madini ya vito ina uwanja mpana wa kujiajiri ikiwa ni kujiajiri katika masuala ya ukataji, ung’arishaji, usonara pamoja na biashara ya madini hivyo anaiona fursa kwa upana pindi atakapoamua kujiajiri. Amesema, Manufaa ya elimu hii ni kubwa sana kwenye biashara ya madini.
Aidha, amewaasa watanzania hususani vijana kutokujihusisha na biashara ya madini ya vito pasipokuwa na uelewa wa kutambua na kuthaminisha madini hayo kwani kufanya hivyo kutapelekea kupata hasara na kupoteza mtaji anaotaka kuwekeza kwani anaweza kuuziwa madini yasiyo halisi kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wafanyabiashara wa madini wasiokuwa waaminifu.
“Serikali imewekeza pesa nyingi kwenye kituo hiki ili kutusaidia kupata uwelewa wa madini ya vito, ni vema tuichukue hii kama fursa kwa kujitokeza kwa wingi kusoma kuliko kufanyabiashara pasipokuwa na elimu hii muhimu” alisisitiza.
Akizungumzia manufaa anayoyapata kutokana na elimu ya sayansi ya madini ya vito Eva Mowo alisema kutokana na kuwa yeye ni mwajiriwa ndani Sekta ya Madini, elimu anayoipata itakwenda kuongezea nguvu miongoni mwa watumishi wengine wanaojikita katika suala zima la uthaminishaji na utambuzi wa madini ya vito.
Amewataka watanzania wengine wenye maono ya kujihusisha na biashara ya madini pamoja na uongezaji thamani wa madini ya vito na miamba kujiandikisha katika kituo hicho ili kupata ujuzi kutokana na chuo kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia pamoja na vifaa vya kutosha vilivyowekezwa na serikali kwa lengo la kuifanya sekta ya madini kuongeza tija kwa wazawa tofauti na ilivyokuwa awali kuwa madini yalikuwa yakinufaisha mataifa mengine ya nje kupitia ajira za uthaminishaji, utambuzi na ukataji wa madini ya vito.
Akizungumzia hatua zinazopitiwa katika suala zima la utambuzi wa madini halisia na yasiyo halisi Mjemolojia Eusebi Bernard amesema utambuzi wa madini unapitia hatua kadhaa zikiwemo upimaji wa uzito (specific gravit), upitishaji wa mwanga(polarization), hadubini (Microscope) pamoja na upimaji wa refractive index.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo Ester O. Njiwa, amesema chuo hicho kinadahili watu wa rika zote ikiwa ni pamoja na wenye elimu ya msingi pamoja na wasomi kwa ngazi ya shahada pia kinadahiri wafanyakazi katika kada mbalimbali wenye nia ya kupanua uelewa katika tasnia ya Elimu ya Sayansi ya Madini ya Vito na Miamba.