Na Mwandishi Maalum
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anayeshughulikia Maendeleo ya Jamaii Dkt. John Jingu amesema Wizara hiyo itahakikisha inatekeleza kikamilifu agizo la Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan la huduma kwa makundi maalum ya watoto na Wazee wasioniweza.
Dkt. Jingu ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipotembelea makazi ya Watoto na Wazee wasiojiweza ya Mama theresa yaliyoko Mburahati.
Amesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo ina dhamana na Wazee na watoto itahakikisha inatekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia taifa kupitia Bunge jijini Dodoma.
“Mimi ndio mtumishi Mkuu kwenye eneo hili na kazi yangu kubwa ni kuhakikisha kwamba maelekezo ya Rais aliyoyatoa wakati akihutubia taifa Bungeni hivi karibuni, yanatekelezwa kwa kasi kubwa” alisisitiza Dkt. Jingu
Ameyahakikishia makundi hayo maalum ya Watoto na Wazee wasiojiweza kuwa wao ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Flora Emmanuel ameeleza kufarijika kutokana na hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya sita kwa kuhakikisha walengwa hao wanaishi katika mazingira bora.
“umetuletea ujumbe mzuri,sio kwetu sisi tu humu ndani bali hata nje. Mwenyezi Mungu akupe baraka na nguvu ya kufanya kazi,” alisema Flora
Akihutubia Taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana vipaumbele vya Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa makundi maalum zikiwemo huduma kwa watoto na Wazee wasiojiweza.