NEWS

25 Aprili 2021

Waziri Mhagama: NSSF Toeni Huduma Bora Zitakazo Wahamasisha Kupata Wanachama Wengi


Na: Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka Viongozi wa Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa NSSF, Mameneja wa Mkoa wa mfuko huo na Maafisa Matekelezo kuongeza juhudi katika kutoa huduma bora na zinazotekelezeka ili kuvutia wanachama zaidi.

Hayo yameelezwa wakati wa kikao kazi kilichokuwa kikiongozwa na Waziri huyo alipokutana na Menejimenti ya Mfuko wa hifadhi ya Jamii wa NSSF, Mameneja wa Mkoa wa mfuko huo na Maafisa Matekelezo “Compliance Officer” lengo ikiwa kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Waziri Mhagama alieleza kuwa, Mfuko unawajibu wa kutoa huduma bora kwa wanachama wake kama vile kukusanya michango yao, kuwalipa mafao kwa wakati, kuwapatia taarifa muhimu zinazohusu Mfuko, kuboresha taarifa za wanachama, kuimarisha mawasiliano baina ya mteja na mtoa huduma, kupokea kero zao na malalamiko na kujibu kwa wakati, kutumia lugha nzuri na zenye staha katika kutoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali.

“Dira yenu yenu inaeleza kuwa mnatoa huduma zinazoaminika na endelevu za hifadhi ya jamii na pia dhima ya Mfuko ni kufikia malengo hayo ya dira kwa kupitia Watumishi wenye ufanisi, ubunifu na ari ya kazi kwa kutumia teknolojia sahihi,”

“Pamoja na malengo hayo mazuri ya mfuko lakini kumekuwa na baadhi ya changamoto ambazo inabidi kuzifanyia kazi ili kupiga hatua zaidi na zaidi katika kufikia dira ya mfuko mnapotekeleza majukumu yenu,” alisema Mhagama

Alieleza kuwa, sehemu yoyote yenye huduma duni huwa msingi wa malalamiko yoyote, hivyo kunapelekea wanachama kulazimika kuwatumia viongozi wa Serikali kuwasilisha malalamiko yao.

“Kutoa huduma bora ni muhimu kwa kuwa kutapunguza malalamiko” alieleza Mhagama

Kutokana na changamoto hiyo Waziri Mhagama aliagiza Menejimenti ya Mfuko huo kujenga utamaduni wa kufuatilia kwa karibu malalamiko na wasipuuze malalamiko yatakayokuwa yakiwasilishwa na Wanachama.

“Watendaji ngazi zote mliopo Makao Makuu, Mameneja wa Mkoa na Maafisa Matekelezo “Compliance Officer” fungueni milango ili mkutane na wananchi wenye shida. Msijifungie na kufanya kazi kwenye makaratasi tu, ni lazima uwepo mfumo ambao utaleta tija katika kuhudumia wanachama,” alieleza Mhagama

Sambamba na hayo, Waziri mhagama alitaka mfuko huo kuandikisha wanachama wapya na waajiri ili kupanua wigo wa hifadhi ya jamii. Mfuko una wajibu wa kisheria kusajili Waajiri na Wanachama kutoka kwenye Sekta Binafsi pamoja na wale wa Sekta isiyorasmi kupitia Mfuko wao maalum wa “National Informal Sector Scheme”.

“Sekta Binafsi na Sekta isiyo rasmi zinazokuwa kwa kasi zaidi kutokana na kupanuka kwa uchumi wan chi yetu, hivyo kundi hilo ni muhimu kulisajili kwenye mifumo yetu ya Hifadhi ya Jamii ambayo itasaidia kufikia malengo ya Sera inayotutaka kuweka mifumo na kuchukua hatua zitakazopelekea kupanua wigo wa sekta hiyo,” alieleza

Aidha aliagiza kuwa Mfuko uje na mkakati wa uhamasishaji na utoaji wa elimu sambamba na ubunifu katika teknolojia pamoja na vitita vya mafao ili kuvutia Sekta Binafsi na Sekta isiyorasmi ili ione umuhimu wa kujisajili kwenye mfuko huo.

Waziri Mhagama alielezea pia suala la uwepo wa baadhi ya Ofisi za mikoa ambazo zimekuwa zikipuuzia kufanya kaguzi mbali na kuwa ni takwa la kisheria, Kanuni lakini hata Miongozo ya ndani utendaji (Compliance Manual) ambayo imeweka ulazima na utaratibu wa kufanya kaguzi hizo kwa kila mwajiri.

“Wengi wenu hamtekelezi hili takwa kwenye mikoa yenu. Ninafahamu pia kwamba baadhi yenu mnachukua rushwa kwa waajiri ili msiende kuwakagua au mnasaini vitabu tu na kuondoka; hakuna hata anayejishughulisha kusema aitiwe wafanyakazi wawili watatu ili awasikilize kubaini maeneo ya ufuatuiliaji. Hali hii imepelekea kuwepo kwa mlundikano wa wanafanyakazi ambao wahawajasajiliwa, au wamesajiliwa lakini michango yao haiwasilishwi NSSF,” alisema Mhagama

Akielezea changamoto nyingine ya kutokukusanywa kwa michango ya wanachama ambalo ndilo tatizo kubwa zaidi hali hii imepelekea walalamikaji hao kushindwa kulipwa, kucheleweshwa au kupunjwa mafao kutokana na kuwepo kwa mlolongo wa michango ambayo haikuwasilishwa.

Aliagiza Mfuko huo uendeshe zoezi maalumu la kukusanya malimbikizo “arrears” ili kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hilo.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa watumishi wote wa mfuko huo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kwa weledi na uaminifu ili kutimiza malengo ya mfuko huo.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza kazi za kusukuma guruduma la maendeleo ya nchi yetu niwaombe sana sana mtoe ushirikiano unaotakiwa ili kufanikisha majukumu ya Mfuko na pia kila mmoja atekeleze wajibu wake,” alisema

Pia Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Masha Mshomba kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuliongoza mfuko huo wa NSSF.

Kikao kazi hicho kilichofanyika katika jingo la NSSF lililopo Ilala kiliudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Jamal Katundu.