Na Richard Mwamakafu, Arusha
Waziri ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Innocent Bashungwa amezitaka taasisi za Barazala la Sanaa la Taifa (BASATA) Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Filamu (TBF) kufanya uhakiki wa kazi za sanaa kwa utaratibu ambao haukwamishi kazi za wasanii nchini.
Mhe. Bashungwa amesema hayo Mei 02, 2021 Jijini Arusha ambapo ameeleza kuwa uhakiki unaofanywa na taasisi hizo lengo lake ni kulinda maadili kwa kuhakikisha maudhui ambayo yapo kinyume na mila na desturi za Mtanzania bila kuathiri ubunifu wa wasanii wetu, maendeleo ya sanaa nchini na kudumaza ukuaji wa ajira.
“Kwa upande wa filamu, uhakiki unasaidia kujua maudhui yaliyopo kwenye filamu husika ili kuamua ipangiwe daraja gani na unasaidia kuepusha maudhui mabaya ya kuharibu maadili ya jamii yetu, yadhibitiwe kabla ya kufika kwa mtazamaji/msikilizaji” amesema Waziri Bashungwa.
Waziri ameongeza kuwa Wizara inaendelea kupokea maoni na kukutana na wadau ikiwa ni sehemu ya namna ya kuboresha chambuzi na hoja zilizowasilishwa ambazo zitasaidia kuziunganisha BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu ili kuleta tija na kusimamia kazi za Sanaa na Wasanii nchini.
Vilevile amewasisitiza wadao ambao hawajawasilisha maoni yao, kuendelea kutoa maoni yatakayosaidia kuwa na Sheria na Kanuni zinazosimamia maudhui ya kazi za Sanaa kupitia taasisi hizo ili yasiende kinyume na mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania.