NEWS

3 Mei 2021

Majaliwa: Tutumie Mweziwa Ramadhani Kumuomba Mwenyezi Mungu Aendelee Kuibariki Tanzania


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasisiza waislam nchini watumie Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Tainzania, viongozi na wananchi wake wadumishe amani na mshikamano.

Ameyasema hayo jana(Jumapili, Mei 2, 2021) katika Fainali za Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur’an yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yahusisha washiriki 15 kutoka nchi 11.

Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa waumini wa dini ya kiislam nchini waendelee kuyaishi mafundisho wanayoyapata katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwenye maisha yao ya kila siku.

 “Natambua mchango mkubwa wa waumini katika kuienzi na kuitunza amani kwa kufuata miongozo ya viongozi wetu kupitia mafundisho ya Qur’an ambayo hututaka kuepuka kuivuruga amani.”

Amesema amani ni matokeo ya msingi imara iliyoachwa na waasisi wa Taifa, hivyo hawana budi kuienzi na kuilinda kwa ajili ya maslahi na mustakabali wa nchi. “Mwitikio mkubwa tunaouona kwenye mashindano haya ni kielelezo cha amani, umoja na mshikamano tulionao.”

Pia, Waziri Mkuu amesema ni vema vijana hao waliohifadhi Qur’an wakaendelezwa kitaaluma katika fani zingine za elimu kwani uwepo wao ni muhimu katika kujenga jamii bora na yenye uadilifu.

Amesema si jambo rahisi kumuona mtaalamu aliyehifadhi qur’an akienda kinyume na maadili ya taaluma yake kwa sababu Qur’an pekee inatosha kumfanya mwanataaluma huyo aonyeke dhidi ya vitendo vinavyokwenda kinyume na uadilifu.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau mbalimbali waunge mkono juhudi zinazofanywa na taasisi mbalimbali za kuhifadhisha Qur’an nchini katika kujenga Taifa bora la vijana wenye maadili na kutoa wataalamu wa fani mbalimbali ambao wana hofu ya Mwenyezi Mungu katika mioyo yao.

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zuber ametumia fursa hiyo kuwahamasisha waumini wa dini ya kiislam kujenga utamaduni wa kuhifadhi Qur’an kwa kuwa ndiyo jambo muhimu kwa sasa.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania, Sheikh Othman Kaporo aliziomba  taasisi mbalimbali za kiislaam kushirikiane katika kuwalea vijana kwenye maadili mema.

Katika mashindano hayo mshiriki kutoka nchini Yemen, Mohammed Abdo Ahmed (22) ameshinda nafasi ya kwanza katika upande wa kuhifadhi qur’an na amepata zawadi ya Dola za Marekani 5,000 na Mohammed Haruna Hassani (37) ameshika nafasi ya kwanza kwa upande wa kusoma Qur’an kwa njia ya tajweed na kupewa zawadi ya shilingi milioni mbili.

(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU