NEWS

1 Mei 2021

Serikali Yafunga mtambo wa kisasa JKCI wenye thamani ya shilingi bilioni 4.6


Serikali imefunga mtambo wa kisasa wenye thamani ya shilingi bilioni 4.6 wa uchunguzi na matibabu ya moyo (Catheterization Laboratory – Cathlab) uliounganishwa na mtambo wa  Carto 3 System 3D &  mapping electrophysiology System  ambao unauwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo.

Fedha za kununuliwa kwa mtambo huo ambao umefungwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) zilitolewa na Serikali mwanzoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana  jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema mtambo huo umeshaanza kutumika, licha ya kutibu mfumo wa  umeme wa moyo pia utafanya uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo, kuweka vifaa visaidizi vya moyo pamoja na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuiwezesha JKCI na kufunga mtambo huu wa kisasa   ambao unauwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo.Kufungwa kwa mashine hii yenye teknlologia ya hali ya juu kutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya moyo ikiwemo mfumo wa umeme wa moyo hapa nchini ”,.

“Tuna wagonjwa wengi ambao mfumo wa umeme wa moyo umekuwa haufanyi kazi vizuri hii ikiwa ni pamoja na  hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake ya  moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida  ambao tulikuwa tunawasafirisha kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutibiwa huku wengine wachache wakipatiwa matibabu hapahapa nchini”, alisema Prof. Janabi.

Prof. Janabi alisema  mtu akiwa na tatizo katika mfumo wa umeme wa moyo ambalo anaweza kulipata kwa kuzaliwa nalo au athali ya ugonjwa linapelekea mfumo wa umeme wa moyo kubadili mapigo yake inaweza kuwa chini ya 60 kwa dakika  na hivyo kusababisha mapigo kuwa chini sana au kuwa juu ya 100 kwa dakika  na hivyo kuufanya moyo udunde kwa haraka. Kwa kawaida mapigo ya moyo huwa ni 60 hadi 100 kwa dakika.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kupitia utaalam wanaoendelea kuupata kutoka kwa wenzao wa nchi za nje ambao wamewatangulia  katika matibabu ya moyo pamoja na kusimikwa kwa mtambo huo wataweza kuwatibu wagonjwa hao hapa nchini  

“Kwa upande wa wataalamu tunao wa kutosha kwani kuna ambao tumewasomesha nchini China na Afrika ya Kusini pia kupitia kambi mbalimbali za matibabu ya moyo ambazo tunazifanya kwa kushirikiana na wenzetu  wa nje ya nchi ambao wanautaalamu mkubwa zaidi yetu kutatusaidia kupata utaalamu wa kutosha na wa kisasa”, alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake Hassan Ally kutoka kampuni ya Biosense webser ambao ndiyo wafungaji wa mtambo huo alisema katika nchi za Afrika ya Mashariki mtambo huo ni wa pili kufungwa hapa nchini ambapo mtambo wa kwanza ulifungwa katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo Mombasa nchini Kenya.

Alisema mtambo huo una teknolojia mpya na ya kisasa ambayo hivi sasa inafanyika katika matibabu ya moyo Duniani na kuzitaja nchi zingine ambazo zimefunga mtambo huo katika bara la Afrika kuwa ni pamoja na  Afrika ya Kusini na Misri.

“Tumeshatoa na tutaendelea kutoa mafunzo kwa  wataalamu wa Taasisi hii ili wajue jinsi ya kuutumia mtambo huu na tutaendelea  kutoa mafunzo hayo kwa nchi zote za Afrika ambazo zimefunga mtambo huu wa kisasa ambao unateknolojia  mpya hapa Duniani”, alisema Ally .

Naye daktari mwanamke pekee hapa nchini ambaye ni mtaalamu mbobezi wa moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky alisema kufungwa kwa mtambo huo kutawasaidia kutoa huduma nyingi zaidi kwa wagonjwa na kuweza kuokoa maisha yao.

Dkt. Maucky alisema tatizo la mfumo wa umeme wa moyo ni moja ya magonjwa wanayokutana  nayo kila siku hivyo basi kuwepo kwa mtambo huo kutawasaidia kutoa huduma kwa wakati kwa wagonjwa wenye matatizo hayo.

“Teknolojia ya matibabu ya moyo inakuwa kila siku kama mnavyoona tumefungiwa mtambo ambao unateknolojia mpya na ya kisasa  hivyo basi ni muhimu kwa daktari kutenga muda wako ili uweze kujifunza kwa njia ya mtandao au kupitia kwa wenzetu ambao wameendelea kimatibabu kuliko sisi kwa kufanya hivyo hautakuwa nyuma ya teknolojia ya matibabu”, alisisitiza Dkt. Maucky.