NEWS

2 Mei 2021

Vijana Wahimizwa Kujiamini Na Kujitambua Kupambana Na VVU /UKIMWI


 Mwandishi Wetu Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dkt. John Jingu, amewataka Vijana balehe hususani wasichana kujitambua na kujiamini kuwa wao ni  nyezo muhimu ya Kupambana na changamoto za maisha ikiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi

Dkt. Jingu ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa mwaka wa wadau wanaotekeleza Afua za VVU na Ukimwi zinazolenga wasichana balehe na wanawake Vijana.

"Naomba wasichana mjitambue na kujiamini kwani ni nyenzo muhimu ya kutatua Changamoto zinazoendana na umri wenu.Jiamini unaweza kupambana na changamoto,ukilegea kidogo ukiteleza unaharibu ramani ya maisha yako,"amesema.

Amesema endapo wakijitambua hawatakuwa tayari kurubuniwa itakuwa rahisi kwenu kukataa vishawishi, hakikisheni mnasema hapana na maana ya kusema hapana ni kuepuka marafiki wabaya na wenye ushawishi mbovu, vitu vizuri huwa vinachukua muda msiwe na papara na kikubwa mlinde ndoto zenu msizipoteze.

Katibu Mkuu huyo amevitaka vyuo na shule hapa nchini kuanzisha madawati ya Jinsia ili wanaopata changamoto na kufanyiwa vitendo vya ukatili waweze kufika kwenye madawati hayo na kupatiwa msaada.

Dkt. Jingu pia ametumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa nguzo Kuu Sita za Ajenda ya kitaifa ya kuwekeza katika Afya ya Maendeleo kwa Vijana Balehe ambazo ni kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa Vijana, kutokomeza mimba katika umri mdogo, kuzuia ukatili wa kimwili na kisaiklojia na kuboresha lishe miongoni mwa vijana Balehe.

Nguzo nyingine ni kuhakikisha watoto wanapelekwa shule na kumaliza masomo yao na kuwawezesha Vijana Balehe kupata fursa za kiuchumi kwa kuajiriwa na kuajiriwa.

Pia Dkt.Jingu amewataka vyuo na shule kuwajengea uwezo  vijana ili kukabiliana na changamoto huku alisisitiza mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Taasisi mbalimbali kuendelee kulilinda na kulisaidia kundi hili na kikubwa tuwekeze kwenye uwekezaji kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania Dkt. Leonard Maboko amesema ni nia ya Serikali kufikisha Afua za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuwezesha vijana kupata fursa za mitaji na ajira ili kuondokana na changamoto za kukubana na vishawishi.

Dkt. Masoko amefafanua kuwa maabukizi ya Ukimwi kitaifa ni wastani wa asilimia 4.7 kiwango alichosema kitapungua kwa kuwalinda vijana walio katika umri hatarishi.

Amesema asilimia 40 ya watu wenye maambukizi ya VVU ni vijana kati ya umri wa miaka 15 na 24 na asilimia 80 vijana hao ni wasichana.

Naye mmoja wa wawakilishi wa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana Mariana Mathias kutoka Mkoani Mbeya ameishukuru Serikali na wadau kuja na afua mbalimbali zinazolenga kuwasaidia Wasichana Balehe na Wanawake Vijana katika kuoambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI kwani imewasaidia vijana wengi akiwemo yeye kujiamini na kujitambua.

“Mimi ni mfano niliwezeshwa kutoa elimu ya fani ya urembo na kupewa vifaa wezeshi vinavyonisaidia kuendesha maisha yangu ya kila siku na hata kuendesha maisha ya familia yangu” alisema Mariana

Mwisho