Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imefanikiwa kukamata kilo 88.27 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine zikiwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado iliyokuwa imetelekezwa barabarani.
Akizungumza leo juni 17, 2021 jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa DCEA Gerald Kusaya amesema dawa hizo zimekamatwa Juni 2 mwaka huu, saa saba usiku katika eneo la Kimara Korogwe kwa ushirikiano wa DCEA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
"Baada ya upekuzi wa kisheria kufanyika ndani ya gari kulipatikana na mifuko mikubwa mitatu aina ya sandarusi (viroba), ndani yake ikiwa na pakti 12 za dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 12.25 pamoja na kontena za plastiki 73 ndani yake kukiwa na dawa aina ya Methaphetamine zenye uzito wa kilo 76.02," amesema Kamishina Jenerali Kusaya.
Aidha, Kamishna huyo ameeleza kuwa upelelezi bado unaendelea ikiwemo kumgundua mwenye gari hilo na mtanadao wake kwani dereva wa gari hilo baada ya kugundua anafuatilia alitelekeza gari hilo na kukimbia.
Kamishina Kusaya ameendelea kuto onyo kwa wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kuacha kwani vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka hiyo vipo macho.
"Ama zao, ama zetu lakini watambue Mamlaka tuko kazi muda wote na lengo letu ni kukomesha kabisa biashara hi haramu. Tunaomba wananchi waendelee kutoa taarifa ili kwa pamoja tushirikiane kukomesha dawa hizo," amesema Kamishna Kusaya.