Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC limefanya ziara kwenye migodi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu Mikoani Mwanza na Geita kujionea namna ya utunzaji wa mazingira na kuhimiza kuongeza juhudi katika kuyahifadhi na kuyatunza mazingira.
Akiongea na Watumishi wa migodi hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka amesema
"Ni muhimu maji yanayotoka migodini yaratibiwe yawe na ubora unaotakiwa kabla ya kuingia kwenye vyanzo vingine vya maji ambayo yanatumika kwenye maisha yetu ya kawaida ili kulinda afya ya binadamu na viumbe hai wengine."
Dkt. Mafwenga ameongeza kuwa mara nyingi miamba inapopasuliwa na kuwa wazi ikitokea imechanganyika na hewa ya oksijeni na maji matokeo yake maji huwa na madini tembo kama vile kopa, shaba, zinc na mengineyo ambayo yakichanganyika kwenye maji yanakuwa siyo salama kwa matumizi ya wanadamu na kwa viumbe hai vingine.
Dkt. Gwamaka alielezea pia ni muhimu kuwepo na ushirikishwaji wa moja kwa moja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira katika kila hatua za ufungaji wa mgodi ili kudhibiti athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza baada ya mgodi kufungwa.
"Niwaombe wenye migodi mpange mipango ya ufungaji migodi kwa kushirikisha Baraza katika kila hatua ya ufungaji ili na sisi tuweze kutoa maoni yetu ya kitaalamu ili inapofika hatua ya mwisho ya ufungaji mazingira yawe salama".
Naye Jerome Kayombo Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Viktoria alisema mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) unasaidia kufanya maandalizi ya kufunga mgodi pindi zinapoanza shughuli za uchimbaji madini, akatolea mfano wa mgodi wa Buzwagi ambapo
mwamba taka unaotokana na shughuli za uchimbaji unawekewa udongo wenye rutuba na kuoteshwa miti mbali mbali jambo ambalo ni zuri katika kuyahifadhi mazingira yetu.
Muhandisi Dkt Befrina Igulu Afisa Mazingira Kanda ya Magharibi amesema katika hatua za ufungaji wa mgodi wa Buzwagi wenye mgodi wanatakiwa kuhakikisha wanarudisha hali ya mazingira kuwa rafiki na salama kwa jamii.
Aidha amewaomba waliokuwa wamiliki wa mgodi kuangalia jinsi gani miundombinu inaweza kutumika katika matumizi mbadala baada ya ufungaji rasmi.
Rebecca Steven Meneja wa Ufungaji mgodi wa Buzwagi amesema tunapofunga huu mgodi wameazimia kurejesha eneo la mgodi katika hali nzuri ya kimazingira, vile vile miundombinu kama majengo yatatumika kwenye matumizi mengine kama hosteli au hoteli.
Bi. Rebecca akaongeza kuwa maji yaliyomo kwenye shimo lililokuwa linatumika kwenye uchimbaji wa dhahabu yanaweza kutumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
Kwenye suala la usalama Bi. Rebecca amesema wataweka ukuta wa mawe kuzuia watu kuingia na kuweka alama mbalimbali za tahadhari.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira linaendelea kufanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini kujionea hali halisi sekta mbalimbali zinavyozingatia sheria za utunzaji wa mazingira.