Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali imepokea gawio la kiasi cha shilingi bilioni 21.8 kutoka Benki ya NMB, ikiwa ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 206 baada ya kodi iliyopatikana katika benki hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango, alisema Serikali inathamini mchango wa Benki ya NMB katika maendeleo ya nchi na kuupongeza uongozi wa benki hiyo kwa jitihada mbalimbali za kuchangia uchumi wa nchi.
“Nimefurahi kusikia kwamba fedha hizo zimeshaingizwa katika akaunti ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Fedha na Mipango mhakikishe fedha hizo zinatumika katika miradi ya kipaumbele ili kutatua changamoto za wananchi,” alisema Mhe. Dkt. Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango ameelekeza mabenki pamoja na taasisi nyingine za fedha nchini kutumia utaalamu na uzoefu walionao katika Sekta ya Fedha kutafuta suluhisho la riba kubwa ili wananchi waweze kupata mikopo na kuweka amana katika taasisi hizo.
Vilevile, Mhe. Dkt. Mpango amezielekeza taasisi nyingine ambazo Serikali ina hisa kuhakikisha zinajiendesha kwa ufanisi na kutoa gawio Serikalini ili kuiwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo na kuonya kuwa Taasisi hizo kushindwa kutoa gawio ina maanisha viongozi wanaoongoza taasisi hizo hawatoshi katika nafasi hizo.
Aidha, Dkt. Mpango amempongeza Msajilli wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka kwa usimamizi wa mashirika ya umma, taasisi pamoja na kampuni 287 na kuwezesha Serikali kupata gawio kulingana na uwekezaji wa hisa na umiliki wa moja kwa moja wa Serikali.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede alisema mwaka 2019 Benki yake iliipatia Serikali gawio la shilingi bilioni 15.2 lakini kutokana na maelekezo ya Mhe. Makamu wa Rais wakati huo akiwa Waziri wa Fedha na Mipango aliiagiza Benki hiyo kuongeza gawio kwa kuboresha huduma zake hatua iliyochangia kupata faida kubwa na kuiwezsha kutoa gawio hilo la shilingi bilioni 21.8 sawa na ongezeko la asilimia 43.
“Tunaahidi kuwa mwaka ujao tutaongeza ubunifu na uwajibikaji zaidi na kuongeza gawio kubwa zaidi Serikalini” Aliongeza Dkt. Mhede
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara ambayo yamechochea mafanikio ya benki hiyo na kuweza kufikisha mtaji wa Sh. trilioni 1.1.
Bi. Zaipuna alibainisha kuwa pamoja na kutoa gawio hilo, Benki yake pia imelipa kodi mbalimbali serikalini zenye thamani ya shilingi bilioni 245 na kiasi cha Sh. bilioni 1.4 kimetumika katika kuwezesha sekta za elimu, afya, elimu kupitia mpango wao wa kutoa huduma kwa jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameupongeza uongozi wa benki ya NMB kwa kusimamia utendaji wa benki hiyo na kufanikisha kupatikana kwa faida kubwa na kuwaagiza kuendelea kudhibiti matumizi, kuongeza mapato na kusimamia vyema mikopo ili mwakani waweze kutoa gawio kubwa zaidi.
Mhe. Dkt. Nchemba aliiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuendelea na juhudi za kusimamia taasisi na mashirika ya umma kwa kuwa ufanisi wa mashirika hayo una faida kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka amesema kuwa kutokana na usimamizi mzuri ofisi hiyo imeendelea kushuhudia maduhuli ya Serikali yakipanda kutoka shilingi bilioni 225.467 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 753.95 mwaka 2019/20, ikiwa ni ongezeko la asilimia 77 na fedha hizo ziliingizwa moja kwa moja katika akaunti ya Ofisi hiyo.
Mwisho.