NEWS

18 Juni 2021

Upelelezi wa kesi moja kati ya tano zinazomkabili Sabaya wakamilika


Upelelezi wa kesi moja ya unyang'anyi wa kutumia silaha kati ya kesi tano zinazomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, umekamilika na kwamba ameanza kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo.

Hayo yamejiri leo Juni 18, 2021, Jijini Arusha wakati kesi yake pamoja na wenzake  ilipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa ajili ya kutajwa tena kwa mara ya pili.

Wakili mkuu wa Serikali,  Tumaini Kweka amemweleza hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya,  Salome Mshasha kuwa upande wa mashtaka umekamilisha upelelezi huo na upo tayari kuwasomea maelezo watuhumiwa.

Mwendesha mashtaka wa Serikali,  Tarsila Gervas amesema Februari 9, 2021 katika mtaa wa Bondeni,   Sabaya akiwa na watuhumiwa wenzake wawili walitenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya kuvamia duka la Said Saad na kuwaweka chini ya ulinzi.

Gervas amesema Sabaya na walinzi wake,  Sylivester Nyingu (26) maarufu Kicheche na Daniel Mbura(38) walitenda kosa hilo baada kumfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi ambaye ni diwani wa CCM kata ya Sombetini na kumuibia 390,000.

Katika tukio hilo wakitumia silaha,  Sabaya na walinzi hao pia wanatuhumiwa kumpiga mateke kumtishia silaha na kumpora simu na Sh35,000 Ramadhani Ayoub. Watuhumiwa hao ambao walikana mashtaka yanayowakabili wanatetea na wakili, Moses Mahuna.

Kwa kuwa makosa hayo hayana dhamana walirudishwa mahabusu gereza kuu la Kisongo baada ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Julai 2, 2021.

Mashtaka mengine manne yanayowakabili watuhumiwa hao ni ya utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, kuomba rushwa na kuunda genge la uhalifu.