NEWS

1 Mei 2014

Katibu Mkuu wa FIFA kutua Tanzania

Semina ya mawasiliano ya CECAFA inatarai kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke, ambaye atawasili nchini kesho Mei 1, 2014

Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka duniani (FIFA), Jerome Valcke.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jerome Valcke anawasili nchini kesho (Mei 1 mwaka huu) ambapo atafungua semina ya mawasiliano kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Valcke ambaye atafuatana na maofisa wengine saba wa FIFA baadaye kesho hiyo hiyo (Mei 1 mwaka huu) atakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huo utafanyika saa 4 kamili asubuhi kwenye hoteli ya Double Tree by Hilton iliyopo Oysterbay, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Afisa Habari wa Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), Boniface Wambura, amesema timu ya taifa ya Malawi (The Flames) inatarajiwa kuwasili pia kesho kuikabili Taifa Stars katika mchezo wa kujipima nguvu utakayochezwa Mei 4 mwaka huu kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Wambura amesema The Flames yenye msafara wa watu 31 itaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Malawi (FAM).
Tayari Taifa Stars ipo jijini Mbeya kujiwinda kwa mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.