NEWS

30 Novemba 2018

MAMA ATEKWA NA NOAH NYEUSI

DAR ES SALAAM: SIMULIZI ya Fatma Manyinja (49), mkazi wa Mbagala – Chemchem, jijini Dar es Salaam, ambayo inaeleza namna alivyotekwa usiku na watu asiowafahamu na mambo aliyofanyiwa, inaweza kukutoa machozi.  Fatma aliyesimulia mkasa mzima mbele ya waandishi wetu, nyumbani kwake juzi, alieleza mengi kuhusiana na kisa hicho ambacho anasema kimemuacha na maswali mengi huku akiishi kwa hofu.

NAMNA ALIYOTEKWA

Akisimulia kwa majonzi, Fatma anasema siku ya tukio Novemba 12, mwaka huu, alikuwa nyumbani kwake amelala, ndipo akashangaa anasikia mlango wake ukigongwa. “Ilikuwa usiku wa saa 7 nimelala, mtaa mzima umetulia kabisa… nikasikia mlango unagongwa, nilipotoka nikakutana na vijana wawili, wakamwulizia mwanangu wa kiume Fikiri. Nikawajibu leo hakurudi,wakasema kwa nini?

“Nikawaambia yeye ni mkubwa wakati mwingine huwa analala kwa rafiki zake. wakaniuliza ukiambiwa amefariki utajisikiaje? Kabla sijawajibu wakaniambia sasa twende huku utajua kama mwanao amekufa au mzima. “Wakanivuta mkono kuniongoza nje. Nilikuwa nimevaa kanga moja tu, kama unavyojua joto la Dar kwa sasa… nikawaomba basi nivae nguo, wakakataa. Walinichukua na kunipeleka katika gari aina ya Noah. Tena walimchukua na mwanangu mdogo mwenye miaka 11, Said ambaye anasoma darasa la nne.

“Nikawaambia naombeni mwanangu abaki, maana anafanya mtihani wa taifa, wakasema hapana, naye anatakiwa kuongozana na mimi. Tukaingizwa mle ndani ya gari na mwanangu. Mle ndani ya gari tuliwakuta watu wengine wawili na mmoja aliwekwa kwenye buti kwa nyuma. Huyo alikuwa akiugulia maumivu makali,” alisema Fatma na kuongeza:

“Tulivyoingia tu garini, mmoja wao akaniuliza kama nawafahamu wale vijana waliokuwemo kwenye Noah, nikawajibu siwajui maana ni kweli siwajui. Wakamwuliza mwanangu, yeye akasema anamfahamu mmoja, anaishi hapahapa mtaani kwetu. Wakawasha gari na kuondoka eneo lile.”

WAPELEKWA JUMBA LA MATESO

Anasema hakuweza kutambua uelekeo wa gari lile, lakini safari yao iliishia kwenye nyumba moja iliyokuwa na uzio wenye ukuta mrefu ambao haukuwa rahisi kwa mtu kutoroka. “Tulipofikishwa kwenye hiyo nyumba wakatuingiza kwenye chumba kimoja… mimi niliwaambia naumwa, nikawaomba maji ya kunywa lakini wakakataa kunipa,” alisema. Alisema badala ya kumsaidia maji ya kunywa kama alivyoomba, wakaanza kumwagia maji mengi ya baridi mwilini hadi akafikia hatua ya kuishiwa nguvu.

“Walianza kuniongelesha maneno ya matusi, baadaye wakanimwagia maji baridi mengi mfululizo. Wakati huo mwanangu sikujua alipokuwa. Nilijisikia vibaya, nikapoteza nguvu kabisa. Baadaye sikujua kilichoendelea tena, nikapoteza fahamu,” alisema. Anasema baadaye alikuja kuzinduka akajikuta yupo katika uwanja ambao hakujua ni wapi, pembeni yake akiwepo mwanaye Said, wakaanza kutembea wakiwa hawana uelekeo.

“Ilikuwa alfajiri, kukianza kupambazuka… tukakutana na msamaria mwema, ambaye tulimsimulia kila kitu, akatupeleka hadi serikali za mtaa katika eneo hilo. Hapo nikapata simu na kumpigia mume wangu ambaye baadaye kulipopambazuka kabisa alitufuata hapo,” alisema Fatma.

Wakati Fatma anazungumza na Amani alikuwa anajiandaa kwenda kuripoti tukio hilo polisi sambamba na kwenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi baada ya kupewa PF 3.

“Yaani hapa yenyewe mna bahati, ndiyo nilikuwa namalizia kujiandaa niende zangu polisi kutoa taarifa. Hapa nilipo sina amani kabisa. Naishi kwa wasiwasi, nikimuona mtu mgeni machoni mwangu nakuwa na hofu, naamini vyombo vya usalama vitatenda haki, maana mpaka sasa sijui kosa langu ni lipi. “Nilidhani labda mwanangu atakuwa amefanya kitu kibaya, lakini kama unavyomuona huyu hapa (anamwonyesha mwanaye Fikiri aliyekuwepo wakati wa mahojiano),” alisema.

FIKIRI AZUNGUMZA

Kijana Fikiri Said (23), ambaye ndiye anaonekana kuwa chanzo cha mambo yote, alipoulizwa na waandishi wetu kama alipata kugombana na wenzake au kudhulumiana alipinga kuwepo kwa jambo hilo. “Mimi sina tatizo na mtu, uliza mtu yeyote hapa mtaani utaambiwa. Mimi zaidi huwa naimba zangu Bongo Fleva, natafuta namna ya kutoka. Siyo mfanyabiashara useme labda nimedhulumiana na watu,” alisema Fikiri.

Alipoulizwa ikiwa anajihusisha na ukabaji au wizi, haraka Fikiri alisema: “Mimi ni mtu mwema, nadili na muziki tu. Mbona mpaka sasa hivi nipo hapa nyumbani salama? Kama ningekuwa na tatizo kwa nini wasije kunichukua mimi hapa nyumbani? Kiukweli mpaka sasa sijui ni nani na kwa nini wamemteka mama yangu.”

Stori: Waandishi Wetu, Amani

INATISHA! Mama Asimulia Alivyotekwa na Wanae usiku wa Manane!

The post MAMA ATEKWA NA NOAH NYEUSI appeared first on Global Publishers.