PENZI ni kikohozi kulificha huwezi! Hicho ndicho kilichotokea kwa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye rasmi ametangaza kuwa mbioni kumuoa mrembo shombeshombe wa Mombasa nchini Kenya anayejulikana kwa jina la Tanasha Donna Barbieri Oketch a.k.a Zahara Zaire. Katika mahojiano na Gazeti la Ijumaa juu ya ishu hiyo mapema wiki hii, Diamond alikiri kuwa kwenye uhusiano na Tanasha ambaye ni mtangazaji wa Redio NRG ya jijini Mombasa, Kenya.
Diamond alisema kuwa, mara baada ya kuachana na mzazi mwenzake ambaye alizaa naye watoto wawili, Princess Tiffah na Prince Nillan, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, wasichana wengi ‘aliowatokea’ na hata Zari mwenyewe hawakulichukulia jambo la ndoa kwa uzito kama alivyofanya Tanasha.
NAMUOA HUYU…
“Tanasha ndiye mwanamke pekee aliyeonesha kujali na uzito juu ya jambo hilo hivyo rasmi natangaza kumuoa huyu,” alisema Diamond na kuongeza: “Ana sifa zote za mwanamke wa kuoa, lakini unajua sisi wanaume wengi huwa tunaangalia sura, umbo na vingine vya mwilini kisha ndiyo inafuata tabia. “Lakini nimejiridhisha kwamba mbali na umbo na mvuto wa kipekee pia ni mwanamke mwenye tabia nzuri.”
KUTAMBULISHWA UKWENI
Alipoulizwa juu ya uwepo wa Tanasha kwenye ufunguzi wa Tamasha la Wasafi Festival mjini Mtwara, Diamond alifunguka kuwa ni kweli alikuwepo, lakini watu wengi hawakumjua kutokana na usiri uliokuwepo wa kumuonesha kabla ya yeye mwenyewe kumtambulisha alipokuwa stejini.
Diamond ambaye leo anaangusha shoo na Wasafi katika Uwanja wa Samora mjini Iringa alisema kesho Jumamosi, Tanasha atamtambulisha kwa wakwe zake. “Nitakuwa na shoo kesho nchini Kenya katika Mji wa Thika ambapo Tanasha atanitambulisha rasmi kwa wakwe zangu,” alisema Diamond.
AWAFUNIKA ZARI, KIM NANA
Diamond alifunguka kuwa alipima mambo yote ya sura, umbo na tabia na akaona Tanasha ndiye anawafunika wote waliopita (akiwemo Zari, Hamisa Mobeto na Kim Nana).
TANASHA NI NANI?
Tanasha ni mrembo mwenye umri wa miaka 22 ambaye ni Mkenya mwenye asili ya Italia. Mbali na utangazaji, Tanasha ni video queen ambaye alishauza sura kwenye Video ya Nagharamia ya staa mwingine wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ aliyoshirikiana na mwanamuziki Christian Bella ‘Obama’.
AKANUSHA PENZI NA KIBA
Kabla ya Kiba kumuoa mrembo Aminah Khalef wa Mombasa, aliwahi kudaiwa kuwa kwenye uhusiano na kutaka kumuoa Tanasha, jambo ambalo mrembo huyo alitoka hadharani na kulikanusha vikali.
“Ningependa kufafanua tetesi ambazo zimekuwa zikiendelea kwenye kurasa mbalimbali za Instagram na blogs zinazonihusu mimi na Kiba. Niseme ukweli kabisa ni za uongo. Kiba na mimi tumefanya kazi pamoja, lakini kamwe hatujawahi kuwa wapenzi,” alikaririwa mrembo huyo mwenye umbo refu, lakini matata kutokana na kujazia kulikopangika.
TUJIKUMBUSHE
Kabla ya Tanasha, Diamond aliwahi kuingia kwenye majaribio mbalimbali ambayo yalifeli. Aliwahi kutangaza ndoa na Zari, mtangazaji, Penniel Mungilwa ‘Penny’, waigizaji Wema Sepetu na Jokate Mwegelo ambazo zote zilifeli.
The post RASMI..DIAMOND KUMUOA HUYU ! appeared first on Global Publishers.