Nteghenjwa Hosseah, Chemba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Selemani Jafo amechukizwa na kusuasua kwa ujenzi wa kituo cha Afya Hamai kilichopo katika Wilaya ya Chemba ambacho hakijakamilika ujenzi wa miundombinu ya Afya ilihali fedha za ujenzi zikiwa zimefikishwa kituoni hapo miezi kumi iliyopita.
Mhe. Jafo ameonyesha kuchukizwa kwake wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Afya inayoendelea kujengwa katika Halmashauri hiyo mapema leo hii.
Akizungumza katika ziara hiyo Mhe. Jafo amesema Kituo cha Hamai kimepokea fedha tangu Januari 2018 lakin mpaka sasa ujenzi haujakamilika wakati vituo vingine vyenye mazingira magumu zaidi vimekwishakamilisha ujenzi tena kwa ubora wa hali ya juu.
Mhe Jafo aliongeza kuwa fedha zilizoletwa hapa ni sh milioni 400 nimeambiwa kuwa zimekwishatumika zote na inahitajika tsh mil 29 zaidi ili kukamilisha majengo haya; Nashindwa kuelewa ni kitu gani cha gharama kilichowekwa katika kituo hiki ambacho kimepelekea fedha hizo kwisha kabla ya ujenzi kukamilika.
“Inakuwaje halmashauri zingine wametumia kiasi hicho cha fedha kukamilisha miundombinu yao lakini kwa chemba fedha hizo zisitoshe kukamilisha kituo kuna tatizo gani hapa” alihoji Jafo
Hakuna fedha itakayoongezwa katika kituo hiki cha Hamai nataka majengo yote yaliyojengwa hapa yakamilike haraka iwezekenavyo na kwa ubora unaotakiwa bila kuwa na sababu zingine zozote mkatafute fedha popote mkamilishe kituo hiki aliongeza Jafo.
Akizungumza na wananchi wa Hamai Mhe. Jafo aliwajulisha kuwa Halmashauri ya Chemba ni miongoni mwa Halmashauri zilizopata fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya vitatu na Hospital ya Wilaya kwa hiyo hatavumilia kuona fedha hizo zikitumika vibaya atasimamia sharia na atakayekwenda kinyume na maelekezo atachkuliwa hatua kali.
Sambamba na kumuagiza Mkurugenzi kutaftua fedha za kukamilisha ujenzi huo Waziri Jafo ametoa muda wa wiki mbili kukamilisha ujenzi huo na ameahidi kurejea tena Hamai mnapo Januri 15,2019 kuja kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
Naye Mbunge wa Chemba Mhe. Juma Nkamia amesema kuwa kumekua na kusuasua kwa ujenzi wa kituo cha Afya Hamai umetokana na ujanja ujanja wa baadhi ya watumishi kutaka kufanya vitu wenyewe bila kushirikisha kamati za ujenzi na mara nyingi wanaposhauriwa hawakutaka kusikiliza ushauri huo ndio baadhi ya sababu zilizochangia kutokamilika kwa ujenzi huo kwa wakati.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba Dkt. Semistatus Mashimba amesema changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa kituo cha Afya Hamai zimetokana na uhaba wa watumishi hususan katika idara ya ujenzi na manunuzi ndio ndio muhimu katika kusimamia shughuli zote za ujenzi wa vituo vya Afya.
Vituo vya Afya vilivyopokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Afya katika Wilaya ya Chemba ni vitatu ambavyo ni Hamai, Mrijo na Kwamkoro ambapo kila kimoja kimepata sh mil 400 huku hospital ya Wilaya ikipatiwa kiasi cha sh Bil 1.5.