NEWS

1 Juni 2019

Ajikata Kidole Baada ya Kupiga Kura Chama Ambacho Hakukidhamiria


Mpiga kura mmoja nchini India amekikata kidole chake baada ya kugundua kuwa alikitumia kupigia kura chama cha siasa ambacho hakukidhamiria.

Kupitia video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, mpiga kura huyo, Pawan Kumar, alisema kwa bahati mbaya aliishia kukipigia kura chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP).

Alisema alitaka kukipigia kura chama kingine lakini alichanganya alama nyingi zilizokuwa kwenye mashine ya kupigia kura.

Kila mpiga kura kidole chake cha shahada huwekwa alama kwa wino baada ya kupiga kura katika taifa hilo.

Kumar alipiga kura yake wakati wa uchaguzi mwezi uliopita katika eneo la Bulandshahr jimbo la Kaskazini la Uttar Pradesh.

”Nilitaka kupiga kura kwenye alama ya Tembo, lakini nikapiga kwenye alama ya Ua kimakosa,” alisema Kumar.

Alielezea alama za vyama zilizokuwa kwenye mashine sambamba na jina la kila mgombea.

Uchaguzi huu unapitia awamu saba, huku kura zikiwa zimekamilika kuhesabiwa Mei 23.

Nchini India kuna wapigakura 900, wanaofanya uchaguzi wa India kuwa mkubwa kuwahi kushuhudiwa duniani.

Wakati BJP alama yake ni Ua, Tembo ni alama ya chama cha Bahujan Samaj (BSP), ambacho kimeungana na vyama vingine viwili kupambana na chama tawala.

Alama za vyama zina nafasi kubwa kwenye uchaguzi wa India kwa kuwa ni rahisi kutambulika kwenye nchi yoyote ambayo yenye watu wengi wasio na elimu.

Lakini pia kuna vyama mbalimbali na muungano wa vyama ambavyo huwachanganya wapiga kura.