NEWS

1 Juni 2019

Makubwa..Mama Mjamzito Ajipasua, Amtoa Mtoto


Mwanamke Joyce Kalinda (30) amezua taharuki kwa wakazi wa Kirando mkoani Rukwa, baada ya kudaiwa kujichana tumbo kwa kitu chenye ncha kali na kumtoa mtoto akiwa hai.

Tukio hilo limetokea jana, baada ya mwanamke huyo kufika kituo cha Afya cha Kirando majira ya saa tisa alfajiri na kuanza kupiga kelele akimtaka muuguzi aliyekuwa zamu ampe huduma za kumsaidia kujifungua.

Imeelezwa kuwa kutokana na kuwepo kwa wagonjwa wengine kituoni hapo, muuguzi alimshauri mama huyo kusubiri kidogo na baadaye atamhudumia lakini aliporejea hakumkuta mgonjwa huyo.

Baada ya muuguzi kutomkuta pale alipomuacha aliamua kwenda getini na kumuuliza mlinzi ambaye alimjibu kuwa mama huyo alitoka nje ya kituo bila kuaga anakwenda wapi.

Kwa mujibu wa Dk. Hashi Mvogogo ilipotimu saa 11 alfajiri mama huyo alirudishwa hospitalini hapo akiwa amepasuka sehemu ya tumbo, huku watu waliomfikisha hospitalini hapo wakiwa wamebeba mtoto mchanga, kwa maelezo kuwa alikuwa amejipasua tumbo na kumtoa mtoto tumboni.

“Tumbo lilionekana kuwa limepasuliwa na kitu chenye ncha kali, alipofika aliwekewa dripu tatu za damu ili kuokoa maisha yake kwani alikuwa amepoteza damu nyingi, lakini pia mtoto amepewa matibabu kutokana na kutolewa tumboni bila kufuata utalaalamu” amesema Dk. Mvogogo.

Hata hivyo Dk. Mvogogo ambaye ndiye mganga mkuu wa wilaya ya Nkasi amesema bado uchunguzi unaendelea kufanyika na tayari wamewaachia Polisi kuendeleza uchunguzi huo ili kubaini iwapo ni kweli alijifanyia upasuaji mwenyewe au alifanyiwa na mtu mwingine.

Aidha amesema uchunguzi utakaofanywa pia utahusisha mtaalamu wa ugonjwa wa akili ambaye atachunguza na kubaini kama mamahuyo ambaye ni uzao wake wa nne ana ugonjwa wa akili au la.