NEWS

1 Juni 2019

Wakuu wa Mikoa Waonywa Kuhusu Matamko Wanayoyatoa


Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwita Waitara amewaonya wakuu wa mikoa ambao wamekuwa wakitoa matamko ambayo yako tofauti na maagizo ya serikali.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma baada ya mkuu wa mkoa wa Iringa, Ali Hapi kutoa tamko la kuwataka waandishi wa habari kuwa na vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo ndogo vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Amesema kuwa tamko lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuhusu makundi yanayotakiwa kupewa vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo si la Serikali.

Aidha, mezitaja sifa za Mfanyabiashara anayetakiwa kupewa kitambulisho kuwa awe na mapato ghafi yasiyozidi Tsh. Milioni 4 kwa mwaka, awe hajawahi kuandikishwa na kupewa namba ya kitambulisho cha mlipa kodi (TIN), pia, awe anatambulika kama Mfanyabiashara ama mtoa huduma mdogo kupitia ofisi ya Mtendaji wa Mtaa ama Kijiji kwa mujibu wa sheria

“Ninatoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa, Watendaji wote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhusu ugawaji wa vitambulisho vya Wafanyabiashara na watoa huduma wadogo.”amesema Waitara

Hata hivyo, ameongeza kuwa vitambulisho 1,176,305 vimegawiwa kwa Wafanyabiashara na watoa huduma wadogo na tayari Tsh. Bilioni 23.5 zimeshakusanywa.