Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini wiki hii walishiriki Semina ya Uelewa Kuhusu Ualbino iliyofanyika mjini Morogoro.
Semina hiyo ilizungumzia umuhimu wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010.
Kupitia semina hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Under the Same Sun (UTSS), wahariri walipata nafasi ya kukumbushana mambo mbalimbali yahusuyo ualbino kwa jumla ikiwemo jinsi mtoto mwenye hali hiyo anavyopatikana, changamoto za hali hiyo pamoja na njia ya kukabiliana nazo.
Akiwasilisha maada kuhusu mapitio ya sheria ya watu wenye ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010, Ofisa wa Sheria wa UTSS, Maduhu William aliwaomba wahariri na wadau ‘kupiga kelele’ ili sheria hiyo ifanyiwe marekebisho kuendana na mazingira ya sasa.
Marekebisho hayo ni pamoja na eneo la ajira ambapo mpaka sasa hakuna kanuni zilizotungwa ili kuwezesha utekelezaji wa jambo hili, lakini pia eneo jingine ambalo linaonekana kutoendana na wakati wa sasa ni kitendo cha sheria hiyo kuruhusu uanzishwaji wa makazi maalum kwa watu wenye ulemavu.
Naye Ofisa Utetezi na Haki za Binadamu wa UTSS, Perpetua Senkoro alisema, kuna umuhimu wa Serikali ya Tanzania kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Haki za Binadamu Afrika kuhusu haki za watu wenye ulemavu Afrika pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha azimio katika harakati za kukomesha madhila na unyanyapaa kwa Watu wenye Ulemavu.
Na Sifael Paul aliyekuwa Morogoro
The post SEMINA YA UELEWA KUHUSU UALBINO KWA WAHARIRI appeared first on Global Publishers.