Na Christopher Philemon
Serikali imesema inafanya ukarabati mkubwa wa reli ya kati inayoanzia Dar Es Salaam kwenda mikoa ya Tabora,Kigoma hadi Mwanza ambao itagharimu takribani dola 300 za kimarekani.
Ukarabati huo umeanza mwaka 2018 utakamilika ifikapo mwaka 2021 na hivyo kurahisisha huduma kwa watumiaji wa usafiri huo wa gari moshi(treni).
Akiongea na waandishi wakati wa ziara ya kukagua ukarabati wa eneo la Kilosa hadi Itigi naibu waziri wa Ujenzi ,uchukuzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye,alisema kuwa ukarabati huo mkubwa unaofanywa ili kuweza kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za jirani kama Uganda na Rwanda.
Nditiye alisema ukarabati huo pia utasaidia kusafirisha abiria kwenda mikoa ya Kigoma na Tabora kwa siku mbili kutoka Dar es Salaam_kigoma ambapo itakuwa tofauti na hivi sasa gari moshi(treni)hutumia siku tatu.
Naibu waziri alitoa wito kwa wananchi na madereva wa magari wanaopita kukatisha reli kuwa makini kwa sababu ukarabati huo treni itakuwa inakimbia kwa kasi ya kilometa 72 kwa saa.
Naye Mhandisi ,Uboreshaji wa Reli ya kati kutoka shirika la Reli Tanzania (TRC) Edwin Leonard alisema uboreshaji wa reli hiyo unafanywa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) inatekelezwa katika vipande vinne ambayo ni Dar es Salaam- Ngerengere- Kilosa – Itigi hadi Isaka na watanzania zaidi ya elfu mbili na wageni miambili na ishirini wamepata ajira.
Baadhi ya wafanyakazi wa kitanzania walioajiriwa katika kampuni hiyo walisema kuwa kazi hiyo inawasadia kupata kipato cha kuendesha maisha yao.
"Kwa kweli tunashukuru ukarabati huu umetupatia kazi na inatusaidia sana sisi kuweza kuendesha maisha yetuna pia tumepeleka watoto shule kwa kazi hii hii"alisema Hamisi Omary
Ukarabati wa reli hiyo unakwenda sambamba na Ujenzi wa madaraja,uinuaji wa tuta la reli pia kujenga vituo vya kudumu vya kusimama trein pindi lifanyapo Safari zake.