NEWS

1 Juni 2019

Zimbabwe Kununua Korosho za Tanzania


Baada ya Zimbabwe kuonyesha nia ya kununua mahindi na mazao mengine kiasi cha 800,000 kutoka Tanzania, taifa hilo la Kusini mwa Afrika linafikiria pia kuanza kununua mazao mengine kama korosho.

Ujumbe kutoka Serikali ya Zimbabwe utawasili nchini kuanzia siku ya Jumanne ya Tarehe 3 Juni na unatajiwa kuwa nchini mpaka tarehe 7 ya Mwezi Juni.

“Ujumbe huo unakuja kwa ajili ya kuangalia na kujiridhisha kuhusu mambo ya msingi kama ubora wa chakula na mambo mengine ya awali,” Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasima hayo jana wakati wa kikao cha dharura na wakurugenzi wa taasisi na idara mbalimbali za Wizara ya Kilimo.

“Zimbabwe imefikiria pia kuanza kununua mazao mengine kama korosho kwa kuwa imeona fursa ya kupata mazao yenye ubora na kwa bei nzuri ipo Tanzania. Baadae mazao mengine ya mbegu za mafuta, jamii ya mikunde, mboga na matunda yataanza kununuliwa na taifa hilo,” aliongeza Waziri Hasunga.


Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kuiuzia nchi ya Zimbabwe mahindi na mazao mengine kiasi cha Tani 800,000.