NEWS

28 Aprili 2020

Atiwa Mbaroni Jijini Mbeya Kwa Kusambaza Taarifa za Uongo Kuhusu Corona

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JOYCE KEPHAS AKYOO @ MANKA [31] Mfanyabiashara na Mkazi wa Stereo Jijini Mbeya kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kuhusu ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu [COVID 19] katika Mtandao wa Kijamii.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 27.04.2020 majira ya saa 13:30 Mchana baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kufanya msako huko eneo la Stereo lililopo Kata ya Manga, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya.

Ni kwamba mnamo tarehe 30.03.2020 majira ya saa 14:09 Mchana mtuhumiwa alituma taarifa za uongo na zenye lengo la kupotosha kuhusiana na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu kwenye kundi “Fans of Mwailubi Car Wash” katika mtandao wa WhatsApp kwa kuweka picha za marobota ya nguo akieleza kwa maandishi na kwa sauti baada ya kujirekodi akisema “Mablanket ya Wagonjwa wa Corona ambao wamefariki nchini China na nguo hizo zinaletwa barani Afrika na ugonjwa wa Corona” Mtuhumiwa aliendelea kuongea na kuandika akitahadharisha watu wasikubali msaada huo.

Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Tangu kuanza kwa Janga la Homa Kali ya Mapafu [COVID 19] na kutangazwa kama Janga la Dunia, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Viongozi wakuu wa Nchi ndio wamekuwa wakitoa taarifa kuhusiana na ugonjwa huo pamoja na namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi yake, hata hivyo Serikali imekuwa ikitoa makatazo mbalimbali kwa wananchi kuacha kutoa taarifa za kupotosha umma na kusubiri kupata taarifa kutoka vyanzo sahihi.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mpaka wa Tanzania na Malawi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, maeneo ya Karantini na kudhibiti magari ya kubeba abiria kwa kuwataka kupakia abiria kulingana na siti zilizopo [level seat].

Pia elimu inaendelea kutolewa kwa Wananchi katika maeneo mbalimbali namna ya kujikinga na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona [COVID 19] na kuwataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi, Wataalamu na Wizara ya Afya ikiwemo kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono [Sanitizer].

Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.