NEWS

12 Septemba 2020

JK, Nape wamnadi Salma Kikwete



 RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete na Mbunge wa Mtama (CCM) aliyepita bila kupingwa, Nape Nnauye, wamemnadi na kumuombea kura Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga lililopo mkoani Lindi, Salma Kikwete.

 Akimuombea kura katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika Viwanja vya Mahakamani vilivyopo Kata ya Milola, Kikwete, aliwataka wapiga kura wa jimbo hilo wamchague mbunge atakayekuwa karibu na watawala ili changamoto na kero za Mchinga zipatiwe majawabu ya ufumbuzi.

 “Nimekuja huku kumsindikiza Salma kwa sababu ni mke wangu ananihusu, namfahamu Salma kwa zaidi ya miaka 30 sasa, ni mke mzuri, ni mama mzuri wa watoto lakini pia ana mapenzi makubwa na jamii, anatumia muda mwingi kufanya shughuli za kijamii hasa za watoto wa kike na kina mama, amejishughulisha na jimbo hili kabla hata hajawa mbunge ili kuiunganisha Mchinga na Serikali, kwa hiyo sina wasiwasi akishinda atakuwa mbunge mzuri,” alisema Kikwete na kuongeza:

 “Mbunge wa upinzani anakosa mnyororo wa ushirikiano kati yake na Serikali kwa sababu anakosa nguvu, huwezi leo jukwaani unatukana halafu asubuhi unamfuata Jafo akusaidie zahanati, kwa hiyo chagueni mbunge atakayekuwa karibu na watawala, mbunge atakayewasemea shida zenu. Sina wasiwasi kwamba CCM itashinda urais, kwa hiyo mkimchagua Salma mtapata kiunganishi kitakachowaunganisha kwa uhakika atakapozungumza na wakubwa, mlimsikia Mama Samia wakati wa uzinduzi wa kampeni za Mchinga kwamba atamsaidia Salma kwa hali na mali, atamshika mkono kuhakikisha changamoto za Mchinga zinapata ufumbuzi.

 “Sasa mkimchagua mgombea mwingine atakutana wapi na Magufuli na Samia, fanyeni uamuzi wa kutafuta majawabu ya changamoto zenu, msifanye uamuzi wa kutafuta majawabu ya changamoto za mtu mwingine.”

 Pia Kikwete alisema pale Salma atakaposhindwa kufika atamsaidia kwa kumshika mkono kwa kuwapigia simu wahusika.

 “Nawahakikishia sitamtupa mkono pale atakaposhindwa, nitamwambia naomba nizungumze nao kwa simu na hawatakataa kupokea simu yangu, hawezi kukataa Magufuli, Samia, Majaliwa au waziri yeyote yule, nitawaambia katika yale mambo kule Mchinga kuna tatizo, hivi mnalijua hili, watasema lipi mzee,” alisema Kikwete na kuongeza:

 “Nitasema kadha wa kadha hebu msaidie mbunge, watasema mwambie aje, Salma atakwenda, nitamfungulia mlango, kwa hiyo ni fursa nzuri, nawaombeni ndugu zangu msiipoteze, mkipata Rais, mbunge bila diwani haijakubalika, figa moja au mawili hayajapika ila mafiga matatu ndiyo yanayopika.”

    Kwa upande wake, Nape, alimnadi Salma kwa kutaja sifa tatu zinazombeba kuwa mbunge wa Mchinga ambazo ni kujua changamoto, kujua wapi kwa kupata majibu na kuwa na uwezo wa kuchukua majibu ya changamoto.

 “Mama Salma anataka Mchinga ifanane na maeneo mengine ya nchi, ubunge sio kazi ya kwenda kujifunza, mtampeleka mtu kwenda kujifunza atamaliza miaka mitano akirudi amemaliza na wenzake wamegawana, na nyie miaka mitano mlimpeleka mtu rehani kwenda kujifunza, jamaa amejifunza amerudi anajua kuvaa suti mwisho wake nyinyi mmebaki na matatizo yenu,” alisema Nape na kuongeza:

 “Sio mnachagua mtu mkilia na yeye analia, mkililia barabara na yeye anapanda jukwaani kutukana, barabara haijengwi kwa kutukana na kuandamana, mchagueni Mama Salma kwa sababu nyinyi mkilia yeye anasema nyamazeni ngoja nikalete majibu. Mchagueni kwa sababu anataka kuukomboa ukanda wa Rutamba, Milola na Kiwawa kwa kuhakikisha hii barabara kutoka Ngongo inapitika kwa mwaka mzima, mkinichagulia Mama Salma tutahakikisha hizi changamoto za barabara zinamalizika.

 “Msichague mbunge kwa ushabiki halafu akija bungeni tumfundishe milango inafungukaje, ila mkimchagua Mama Salma anajua matatizo ya Mchinga, hapa Milola anajua mna tatizo la huduma za afya na mnastahili kituo cha afya ili tuache kuteseka, anajua kuna tatizo la maji atalishughulikia, anajua kuna tatizo la mtandao wa simu atashughulikia, kwa hiyo Oktoba 28, mwaka huu msifanye makosa, mchagueni Rais, mbunge na madiwani wa CCM, Mchinga mna kazi ya kumchagua mbunge atakayeleta majibu ya changamoto zenu.”

 Pia Nape alisema ameteseka kufanya kazi kwa miaka mitano na mbunge ambaye hatoki naye chama kimoja na hiyo ikasababisha kila wakipanga mipango hakuna kilichofanyika.

Naye Salma alisema changamoto zote za Mchinga anazijua na aliwaambia wapiga kura kuwa wao ndio wenye uamuzi wa kuchagua maendeleo ya jimbo hilo katika sekta ya afya, maji, kilimo, nishati, elimu, barabara, uvuvi au kuyakataa.

 “Kero zote nazijua labda zile ndogo ndogo sana lakini nitapita maeneo yote wakati wa kampeni na kukutana na wananchi ili nijue shida zao, tutakutana na Tanroads na Tarura ili kumaliza changamoto za barabara ziweze kupitika kwa muda wote.

 “Kuhusu mawasiliano nimeongea na waziri mwenye dhamana na sasa eneo la Kiwawa wataweka mnara wa simu ili watu waweze kuwasiliana na baada ya muda tatizo hilo litakwisha, kwa hiyo nawaomba wana Mchinga ikifika Oktoba 28, mwaka huu tufanye uamuzi wa busara kwa kumchagua Magufuli, mimi na madiwani wote wa CCM ili tupate maendeleo,” alisema Salma.

 Katika hatua nyingine, alisema katika jimbo hilo mambo mengi yalisimama na umefika wakati sahihi wa kutafakari na kufanya uamuzi wa busara wa kumchagua yeye ili akashughulie changamoto za jimbo hilo.

 “Tumepiga marki taimu kwa muda mrefu, sasa wakati ni huu, kata zote za Mchinga zina changamoto na ili tuzitatue tupeni majembe tufanye kazi, najua walimu hawatoshelezi, barabara hazipitiki muda wote, nipeni kura nikashughulike nazo,” alisema Salma. 

 Mbunge wa Mtama (CCM) aliyepita bila kupingwa, Nape Nnauye (kulia), akimnadi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete, wakati wa mkutano wa kampeni zilizofanyika Viwanja vya Mahakamani katika Kata ya Milola mkoani Lindi jana.