MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema hakuna mtu anayeweza kumuondoa kwenye timu hiyo kwa sasa.
Mo ambaye anafahamika kama mmoja kati ya mashabiki kindakindaki wa timu hiyo, amesema anaamini baada ya muda mchakato mzima wa uwekezaji utakamilika, lakini pamoja na watu kuwa wanazungumza mambo mengi, yeye hajali na hawezi kuondoka.
Akizungumza na Spoti Xtra jijini Dar es Salaam jana, bilionea huyo alisema kuwa anaamini asilimia kubwa ya watu wa Simba wanampenda na yeye ana nia njema na timu hiyo, hivyo hatishiki na wachache ambao wanampiga vita.
“Kuna mambo mengi sana yanaendelea, lakini jambo la msingi ni kwamba sina mpango wa kuondoka kwenye timu hii kwa sasa.
“Naamini kuwa kuna watu wana maneno yao, lakini wale wa Simba bado wanani-unga mkono na wana-taka niendelee kukaa hapa, nami napenda kuwaambia kuwa nipo na nitaendelea kuwepo labda hao wenye Simba yao waniondoe, lakini mimi siwezi kuon-doka hata siku moja,” alisema.
Mo amesema kuhusu uwezo wa mtendaji mpya wa timu hiyo, Barbara Gonzalez na anaamini kuwa atafanya kazi nzuri kwa kuwa alipitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba na siyo yeye kama inavyodaiwa.
“Barbara amekuwa chini ya Senzo Mazingisa (CEO aliyepita), kwa kipindi chote na amefanya kazi nzuri, mimi naamini ataendelea kufanya kazi nzuri na watu wanatakiwa kufahamu siyo mimi niliyempitisha kuwa CEO bali ni Bodi, kila mmoja alisema anafaa kwa kuwa wanamuamini,” alisema Mo ambaye ameiongoza Simba kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu na kuwafikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/19