NEWS

10 Septemba 2020

Afya Ya Wema Sepetu Wingu Latanda



NINI kimemkondesha msanii Wema Sepetu? Majibu ni mengi kuzidi swali lenyewe kiasi cha kufanya afya yake kuleta wingu zito miongoni mwa mashabiki wake.



Imeelezwa mara kadhaa kuwa, kukonda kwa msanii huyo aliyepata kuwa Miss Tanzania 2006, kumetokana na upasuaji wa kukatwa utumbo aliofayiwa nchini India wenye lengo la kumfanya apungue baada ya kunenepeana.



Hata hivyo, mwenyewe amekuwa akisema “hali hiyo inatokana na msongo wa mawazo unaotokana na mambo ya kimapenzi.



”Ingawa wembamba siyo ugonjwa lakini histori ya “kufungashia” aliyonayo msanii huyo huenda ndiyo inayomtesa, kwani wengi wamekuwa wakimtazama kwa mtazamo hasi.



“Jamani hivi huyu dada ana tatizo gani, webamba huu siyo bure, kimbunga kikipita si kinaondoka naye,” aliandika mtu mmoja kwenye mtandao wa Instagram ambako picha ya Wema ‘aliyekonda’ ilipostiwa.



Hata hivyo, msanii huyo amekua akikerwa na kauli za “umekonda” ambapo mara kadhaa amekuwa akiwajibu vibaya mashabiki wake wanaomsema hivyo.



“Naugua virusi vya HIV ndiyo maana nimepungua kilo,” Wema alimjibu hivyo shabiki yake aliyekomenti kwenye ukurasa wake wa Instagram baada ya msanii huyo kuposti picha, Februari mwaka huu, akiwa na dada yake na shabiki kumwambia kuwa “amekonda.



”Katika kuonesha kwamba watu wanampenda “Wema bonge nyanya” wengi wao wamekuwa wakitafsiri kukonda kwake na tatizo la kiafya kiasi cha kutamani arudie mwili wake wa zamani.



“Wema wa zamani alikuwa akipita mtaani watu wanajipanga foleni kumshangaa jinsi alivyokuwa kafungashia.“Leo wakitoka watamshangaa jinsi alivyokonda na kubaki mifupa,” aliandika mwingine kwenye mtandao wa kijamii.



Februari 4, mwaka jana kupitia mahojiano maalumu na mwandishi wetu kuhusu kukonda kwake msanii huyo alisema:“Yaani hujui tu ninavyoufurahia huu mwili wangu wa sasa, nimekuwa siyo mzito tena, navaa nguo ambazo nataka na ninapendeza zaidi tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, kwa kifupi najipenda hivi nilivyo.”Ingawa mrembo huyo anasema anajipenda jinsi alivyo, wanaompenda zaidi bado wanatatizika na kukonda kwake.



Mara kadhaa kumekuwa kukienezwa taarifa zisizokuwa na ukweli kwamba Wema amekuwa akidondoka na kupoteza fahamu huku kukonda kwake kukihusishwa na hali hiyo.Hata hivyo, mwenyewe amekuwa akikana kutokewa na hali hiyo na kusisitiza kwamba yuko sawa kiafya.



Daktari Fredrik Mashili kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili amewahi kuwaonya watu wanaotumia dawa kwa lengo la kupunguza miili yao na kuwataka wawe makini.



“Baadhi ya watu wanatumia dawa za kupunguza uzito bila kupata ushauri wa wataalamu, pia sina uhakika sana ila dawa nyingi za kupunguza uzito nchini kwetu hazijapata vibali, nyingi ni dawa za mtaani ambapo kiukweli zingine si dawa za uhakika au zinatumia njia ambazo si sahihi.



“Kuna watu wanazitumia na kuona kuwa wanapungua mwili kumbe wana sinyaa na hivyo kuwa katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya,” Dokta Mashili anasema.



Uchunguzi unaonesha kuwa Wema amekuwa akizidi kupungua kadiri siku zinavyozidi kwenda, jambo ambalo linawafanya watu wapate hofu juu ya afya yake.



Agosti 2, mwaka jana kupitia ukurasa wake wa Instagram Wema aliandika hivi: “Daaaaah kutokana na Comments za watu wengi, inaonekana wengi wanasema ninenepe tena jamani… Ila si ni nyinyi mlonisema nimekuwa Boooooongeee na ilibidi nipungue…



Leo nimeamini Binaadam hamna jema.“Anyways, I will soon Share The Secret to my weight loss na Msijali nitajitahidi kula kula kidogo ili niongezeke hata kidogo tu… Just so you know nilikuwa nina 109kgs na sasa nina 68kgs.”Hayo ni maneno ya Wema mwaka jana lakini kwa kipimo cha macho kisichokuwa na uhakika huwenda msanii huyo amepungua zaidi ya alivyokuwa wakati anaandika komenti hiyo.Kipi cha kushika kuhusu kukonda kwa Wema, linabaki kuwa wingu hakuna wa kulishika zaidi ya kulitazama jinsi linavyochukuliwa na upepo.

Stori: MWANDISHI WETU, Dar