NEWS

14 Juni 2021

CCM Yavunja Ukimya Kuhusu Katiba Mpya


✓Yasema kwa sasa sio kipaumbele chake.
✓Yajielekeza katika kujenga nchi kwanza


Na Mwandishi Maalum kutoka Tanga.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakina  agenda ya katiba mpya kwa wakati huu badala yake kipaumbele zaidi kimewekwa katika kujenga  nchi kwa ukamilishaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, kupambana na umasikini, kuboresha huduma za kijamii, kuboresha mazingira ya biashara, kuzidisha ustawi wa demokrasia, kusimamia utawala bora, kulinda sambamba na kuheshimu haki za binadamu.

Hivyo hakiwezi kuacha masuala hayo ya msingi yaliyobeba mustakabali wa Taifa na kuanza kurudi nyuma kimaendeleo kwa maslahi  binafsi ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo wakati akizungumza na wazee mbalimbali wa wilaya ya Tanga mjini katika ukumbi wa halmashauri ya Jiji la Tanga.

Amefahamisha kuwa Serikali ya Rais Samia inakimbizana na vipaumbele vya msingi zaidi katika maeneo mtambuka ya upatikanaji wa huduma bora  za afya, utoaji  wa elimu bure na bora mashuleni na vyuoni, huduma za maji safi na salama zikiimarishwa katika maeneo hasa yasiyo na huduma hiyo,  kuimarishwa kwa mfumo wa utoaji haki, kutoa  mikopo ya riba ndogo na masharti nafuu, kuboresha  kilimo na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya mazao  sambamba na kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabishara na wawekezaji huku mkazo zaidi ukielekezwa katika  kukomesha rushwa na ubadhirifu jambo ambalo litasaidia katika  matumizi yenye tija ya utajiri wa nchi kupitia rasilimali zake.

"Hakuna mwananchi anayesema serikali iyaache yote hayo ishughulike kwanza na katiba mpya hayupo. Madai ya katiba mpya sio agenda ya kisiasa hivyo wanasiasa waache kuitumia agenda hiyo kama turufu ya kuwahadaa wananchi kuwa hilo ndio jawabu la changamoto zao jambo ambalo sio kweli" alisema Shaka

Shaka alibainisha kuwa Taifa linahitaji viongozi waadilifu, wazalendo, wanaothamini utaifa wetu, wanaotanguliza na kuweka mbele maslahi ya Taifa ili kuwanufaisha wananchi sio wanasiasa mahiri wa propaganda za kutafuta ushawishi wa kutafuta kuungwa mkono kisiasa bila kujenga misingi madhubuti.