Georgina Misama – MAELEZO
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania wote nchini wanaopatiwa huduma za maji kujenga utamaduni wa kulipa bili zao kwa wakati ili Serikali itumie fedha hizo katika miradi mingine ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kurejesha fedha za mikopo.
Akiwahutubia wakazi wa Misungwi Mkoani Mwanza, wakati wa ufunguzi wa mradi wa maji safi na salama na usafi wa mazingira Rais Samia amesema kwamba mradi wa usambazi maji ni ghali na umefanikishwa kwa fedha za ndani lakini pia kutokana na mkopo, hivyo amewataka wanufaika wajenge tabia ya kulipa huduma hiyo ili Serikali iweze kulipa deni hilo.
“Natoa wito kwa Wanamisungwi na watanzania wote kwa ujumla wanaopatiwa huduma za maji, kulipa bili zao kwa wakati kwani kutekeleza miradi ya maji ni ghali sana, na ndio maana sekta binafsi hazijihusushi na miradi hii”, anasema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amezitaka Mamlaka zinazojihusisha na huduma hiyo kutowabambikizia wananchi bili kubwa za maji ili waweze kulipa bili halali kutokana na matumizi yao, kushindwa kufanya hivyo kutawafanya wakwepe kulipia maji hayo na Serikali itapata hasara.
“Msibambikize bili za maji, mpeni kila mtu na anachostahili mkiwabambikiza wakishindwa kulipa watatafuta njia za kupata maji bila kulipa itasababisha Serikali kupata hasara. Wananchi wakiweza kulipa, Serikali itaweza kulipa mkopo huu na kujenga uaminifu ili tuweze kupata mkopo mwingine na tuendeleze miradi mingine ya maendeleo”, alifafanua zaidi.
Kwa upande mwingine Rais Samia, anazitaka Mamlaka zinashughulikia maji Nchini ikiwepo Wizara ya Maji na Taasisi zake, kutumia wataalam wake vizuri ili kuhakikisha wanasambaza huduma hii ya maji kwenye Mikoa na Wilaya zote zenye uhitaji ili kutimiza ahadi ambazo Serikali ilitoa kwa wananchi hao, lakini pia kutimiza lengo la sita katika Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) linalotaka Upatikanaji wa maji safi na salama kwa watu wote.
Rais Samia anasema kwamba katika Wilaya za Mkoa wa Mwanza kuna miradi mingine kadhaa inayoendelea ambapo miradi yote itakapokamilika itatumia kiasi cha fedha cha shilingi bilioni 30.8 ambapo ameziagiza mamlaka zinazohusika, kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa kwani itafanya upatikanaji wa maji kuongezeka na kufikia asilimia 85.
Wakati huo huo amewataka wakazi hao kulinda miundombinu hiyo inayowekwa katika usambazaji maji lakini pia kulinda vyanzo vya maji na kuwa rafiki wa mazingira ili yawatunze.
Vile vile Rais Samia anawataka Watanzania kujifunza utamaduni wa kuvuna maji ya mvua kwa kujenga mabwawa, marambo, visima na matenki ya kuhifadhia maji kwani Tanzania imebahatika kupata maeneo mengi yenye mvua za kutosha lakini maji hayo kwa kiasi kikubwa hutiririka baharini na kwenye maziwa.
Mradi wa maji wa Misungwi umeghalimu shilingi bilioni 13.77 ambapo una uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 4.5 na umehusisha Wilaya za Lamadi na Magu ambapo utatoa huduma kwa watu wapatao 64,208, na hiyo itafanya watu wa Misungwi kupata maji kwa asilimia 100 ukijumuisha maji yanayopatikana sasa hivi. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Benki ya Uwekezaji wa Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo la Ulaya (AFD).