Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Miongoni mwa Vipaumbele vilivyoainishwa na Wizara ya Kilimo katika bajeti ya Mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa bungeni tarehe 24/25 Mei 2021 ni kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ambao unategemea zaidi mbolea.
Katika utekelezaji wake, Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameendelea kukutana na wadau wa makundi mbalimbali, kwa ajili ya kujadiliana juu ya uhitaji mkubwa wa ununuzi na uuzaji wa mbolea nchini.
Akiwa Jijini Dar es salaam kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja tarehe 14 Juni 2021, Waziri Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mhe Hussain Ahmad Al Homaid, Balozi wa Qatar nchini Tanzania na Ndg Abdul Aziz Hamad Alasim, Kaimu Balozi (Head Of Mission) wa Saudi Arabia nchini Tanzania.
Waziri Mkenda ameeeleza dhamira ya serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Pamoja na mambo mengine Waziri Mkenda ameeleza juu ya uwezekano wa makampuni ya nchi hizo mbili kuja kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea nchini kwa ajili ya kutatua changamoto ya mbolea nchini.
Aidha, Uwepo wa viwanda hivyo nchini itaimarisha upatikanaji wa mbolea kwa wingi, kwa bei nafuu na urahisishaji wa huduma hiyo kwa wakulima nchini.
Kadhalika, Waziri Mkenda amepenyeza hoja yake ya kuomba ushirikiano katika nchi hizo mbili ya kuingia katika soko mazao ya mboga na matunda ikiwemo mchele ambayo yanazalishwa kwa kiasi kikubwa nchini.
Waziri Prof. Mkenda kwa nyakati tofauti amewaeleza mabalozi hao kuwa nchi imetangaza nia ya kuuza mbolea (Tender) katika nchi mbalimbali ziweze kushiriki katika mchakato huo wa uuzaji wa mbolea.
Hivyo ili kutanua wigo wa washiriki katika mchakato huo, Ameeleza kuwa serikali imeongeza muda kwa wadau na makampuni kutoka katika nchi hizo kushiriki nia ya kuuza mbolea (Tender).
Katika nyakati tofauti za mazungumzo hayo wadau hao wameahidi kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wan chi zao na Tanzania katika sekta ya kilimo.