NEWS

11 Januari 2014

Mwanamke mwenye miaka 48 akamatwa akiwa amejificha kwenye begi ili aingie Marekani kinyamela

Ndege mjanja hunaswa kwenye tundu bovu, unaweza kutumia akili nyingi kufanikisha tukio lako haramu na bado ikageuka kuwa kituko cha ajabu pindi utakapokamatwa!

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 48, raia wa Thailand alikamatwa na maafisa wa idara ya uhamiaji na mipaka wa Marekani katika mpaka wa Marekani na Mexiko akiwa amejificha/amefungiwa ndani ya begi la nguo ili aweze kuingia Marekani kinyamela.

Maafisa uhamiaji wa Marekani waliweka wazi picha zinazomuonesha mama huyo aliyefahamika kwa jina la Pornkamol Mongkolsermsak akiwa kwenye begi lililokuwa nyuma ya gari lililokuwa linajaribu kuvuka mpaka.


Msemaji wa CBP (Customs and Border Protection), Victor Brabble aliiambia CNN kuwa tukio hilo lilitokea December 30 wakati maafisa walipolishtukia gari aina ya SUV na kulifanyia ukaguzi kwa mara ya pili, ndipo walipomkuta mama huyo akiwa amejificha chini ya nguo ndani ya begi.

Hata hivyo maafisa hao hawakulitaja jina la dereva wa gari hilo aliyetajwa kuwa na umri wa miaka 56, na wawili hao walifunguliwa mashitaka.