Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete |
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa viongozi hao wawili wameifanyia Tanzania mambo mengi, mambo makubwa na mambo ya kihistoria kiasi cha kwamba Watanzania wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa namna ya kudumu.
Akizungumza na Wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari usiku wa juzi, Jumatano, Aprili 16 katika mahojiano maalum ya kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano, Rais Kikwete amesema:
“Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yoyote kuwatukana, kuwadhihaki ama kuwakejeli waasisi wa Taifa letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi yetu mambo makubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mzee Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale Tanzania Visiwani, pengine watu wamesahau, lakini hata pale walipokuwa wanashinda uchaguzi bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Ni ukosefu wa adabu kwa yoyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.”
“Mzee Nyerere yule ametuachia Taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye ndiyo imeendelea kuongoza Taifa letu kwa miaka yote hii. Viongozi wengine wote ambao wamemfuata yeye – Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na sasa mimi mwenyewe, tumefuata na kuongozwa na misingi hii. Na siku nchi yetu inaamua kuipuuza misingi hiyo, tutaingia katika matatizo makubwa.”
Rais Kikwete ametoa msimamo huo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu matusi, kejeli, dhihaki ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalum la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na Wabunifu Wakuu wa Muungano wa Tanzania.