NEWS

1 Juni 2019

Ujenzi wa stendi,soko la kisasa Njombe wamkosha Jafo

Na Amiri kilagalila-Njombe
Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa OR Tamisemi Selemani Jafo amepongeza kuanza kutumika kwa kituo kipya cha mabasi Njombe mjini kinacho iwezesha halmashauri hiyo kukusanya shilingi laki nane kwa siku licha ya kuanza kutumika wiki tatu zilizopita.

Jafo ametoa pongezi hizo mkoani Njombe mara baada ya kufika na kukagua maendeleo ya ukamilishwaji wa kituo hicho  kipya cha mabasi kilicho anza kutumia mei 11 huku baadhi ya maeneo ndani kituo hicho yakiendelea kukamilishwa.

“Ninachofahamu kama mmeanza kukusanya shilingi laki 8 kwa siku,tena stendi ndio kwanza ngeni inaanza na mmeniambia ndani ya wiki moja mmekusanya milioni tano maana yake kwa mwezi mnawastani sio chini ya shilingi ya milioni 20 na kwa mwaka mkiendele itakuwa sio chini ya milioni 240 kwa kitega uchumi hiki kimoja na maana yake  itakapoanza kufanya kazi vizuri itafika muda mnaweza mkakusanya hata milioni 20 kwa wiki”alisema Jafo

Kuhusu ujenzi wa soko kuu la mjini Njombe Waziri amesema kuwa soko hilo ndio litakuwa lakisasa kwa kanda nzima na limejengwa kisasa na kumtaka mkandarasi kukamilisha kwa muda ili liweze kukamilika.

“Hapa ninyi soko mnatengeneza zuri sana tunajenga masoko haya maeneo kadhaa,tunajenga Dodoma tunajenga Mtwara  lakini kwa hili nimeridhika isipokuwa nendeni kwa mda huo, mwezi wa kumi kazi iwe imekamilika,Naomba niwaambie katika hii kanda, Njombe ninyi ndio mtakuwa na soko zuri tena la kisasa na mkandarasi amefanya kazi nzuri mimi nimeridhika nalo sana”aliongeza Jafo

Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa stendi mhandisi Tembo David amesema stendi hiyo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 96,huku akiahidi kukamilisha sehemu zilizobakia za ujenzi kabla ya june 30.huku changamoto kubwa kwa sasa ikiwa ni msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani VAT kwa kuwa mpaka sasa wakandarasi hawajapata.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Iluminata mwenda ameahidi kusimamia kazi kwa nguvu ili kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati.

“Mheshimiwa waziri ameona kazi zetu na tumemueleza changamoto na ametoa maelekezo ya muda wa kumaliza kazi na sisi kuanzia sasa tutasimamia hii kazi kwa nguvu sana”alisema Iluminata Mwenda.