Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi leo Mei,31,2019 imewasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 ambapo inatarajia kukusanya Sh.Bilioni 180 .
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara 2019/2020, bungeni jijini Dodoma,Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi amesema Wizara yake inatarajia kukusanya Sh.Bilioni 180 kutokana na kodi ya pango la ardhi,ada na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi.
Waziri Lukuvi amesema lengo la ukusanyaji wa fedha hizo litasaidia kufanikisha mikakati mbalimbali ya wizara ikiwemo kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya Utunzaji wa kumbukumbu na kuboresha taarifa za ardhi,kurahisisha ukadiriaji wa pango la ardhi na tozo mbalimbali,kutumia mfumo wa kielektroniki na kuendelea kutoa elimu kwa umma.
Aidha,Waziri Lukuvi amesema,katika mwaka 2018/2019 Wizara iliidhinishiwa Sh.Bilioni 65.98 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya Maendeleo ,kati ya hizo,Sh. Bilioni 17.68 ni kwa ajili ya mishahara ,sh.bilioni 17.76 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo n ash.bilioni 30.54 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.
Waziri Lukuvi amefafanua,baada ya uhakiki wa Madeni uliofanywa na Wizara ya Fedha na Mipango ,Wizara ilipewa Sh.bilioni 12.8 kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni na hivyo kuifanya bajeti ya Wizara kuwa Jumla ya Sh.Bilioni 78.8 hadi kufikia tarehe 15 Mei,2019.
Katika hatua nyingine,Waziri Lukuvi amesema hadi kufikia tarehe 15,Mei,2019 ,wizara imeandaa na kusajili hati za hakimiliki 47,688 na kusajili nyaraka nyingine za kisheria 25,045 chini ya sheria ya usajili wa Ardhi huku Wizara ikitarajia kusajili Hatimiliki na nyaraka za kisheria 152,000.
Katika utatuzi wa Migogoro ya Ardhi hapa nchini kupitia kauli mbiu ya Funguka na Waziri , Waziri Lukuvi amesema Jumla ya Malalamiko 13,055 yalipokelewa na malalamiko 10,174 yamefanyiwa kazi na 2,719 yanaendelea kufanyiwa kazi.